Serikali imewatoa hofu waganga wanaojihusisha na utoaji wa huduma za tiba mbadala na tiba asilia nchini na kuwaeleza kuwa hakuna mpango wowote wa kufuta huduma wanazozitoa kama ilivyoanza kudaiwa na baadhi ya watu.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu alisema serikali inatambua namna ambavyo wananchi wa mjini na vijijini wanavyotegemea huduma hiyo hivyo si kweli kwamba wanataka kuifuta bali wanataka watoa huduma hiyo wafuate sheria na taratibu za utoaji tiba.

“Takwimu zinaoenesha kwamba asilimia 70 ya wananchi waishio mijini na asilimia 80 ya waishio vijijini wanategemea tiba mbadala na tiba asilia,” alisema Ummy.

Aliongeza kuwa wizara iliamua kupiga marufuku matangazo yote ya tiba asilia na tiba mbadala kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari kwa kuwa sheria na kanuni za Tiba asilia na Tiba Mbadala zinakataza kujitangaza.

“Kanuni namba 10 ya sheria hiyo inawataka waganga kutotoa tangazo lolote la kuhamasisha watu watumie dawa zao isipokuwa limethibitishwa na Baraza la Tiba asilia na Tiba Mbadala, lakini ilivyo sasa wengi hawayaleti matangazo,” alisema Ummy.

Alisema kuwa wizara yake imekuwa ikipokea malalamiko ya wananchi wengi kuhusu kutapeliwa na baadhi ya watoa tiba asilia na tiba mbadala na ndio sababu ikawataka kuhakikisha wanajisajili kwa mujibu wa sheria ili iweze kuwahakiki na sio vinginevyo.

“Kama kuna wadau wamekwazwa na tamko la wizara, mimi niko tayari kuwasikiliza. Tujadiliane, tuanze agizo la kwanza linasemaje. Tukae mezani… agizo la kwanza linasema wajisajili, waniambie kwanini wasijisajili au kuna changamoto gani zinapelekea wasijisajili,” alisema Ummy Mwalimu.

Kwa upande wa Baraza la Tiba Asilia na Tiba Mbadala, Kaimu Msajili wa baraza hilo, Mboni Bakari alisema kuwa baadhi ya watoa huduma ya tiba asilia akiwemo Dk. Mwaka wamejisajili kurusha matangazo ya tiba zao lakini huvunja masharti wanapokuwa kwenye vyombo vya habari.

“Kwa mfano Dk. Mwaka amesajili kurusha matangazo na baraza limepitia, lakini jambo la kushangaza anapokwenda kurusha hewani kipindi huwa sio ile CD aliyotuletea tukapitisha… jambo ambalo linatushangaza,” alisema Bakari.

Yabainika: Hii Ni Nchi Pekee Duniani Ambayo Magaidi wa ISIS Wanaiogopa
Mchungaji Alazimishwa Kuoa ‘Maiti’ Ya Kiongozi wa Kwaya Aliyempa Mimba