Serikali imeweka mpango wa kuboresha mazingira ya Biashara na uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi mpango unaolenga kurahisisha vibali na upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Viwanda na maeneo ya Kilimo.

Hayo yamesemwa Jijini Dar Es Salaam na  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki wakati akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC, baada ya kupokea ujumbe wa raia saba wa Hongkong China waliowasili Nchini wakiwawakilisha wafanyabiashara wa nchi hiyo waliokuja kufanya utafiti wa maeneo ya kuwekeza.

Amesema kuwa hivi sasa Wizara yake iliyopo Chini ya Waziri Mkuu imeanza kuufanyia kazi mpango huo ambapo pamoja na kuimarisha uchumi wa Nchi kwa kuingiza fedha za kigeni pia utaongeza ajira kwa Watanzania.

“Sisi kama Serikali lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunaimarisha uwekezaji, mpango huo ambao ulifanyika mwezi Mei mwaka jana unalenga kuondokana na vikwazo vya kibiashara na kuharakisha vibali na kutoa ardhi kwa ajili ya uwekezaji, tunayafanya haya ili kuongeza ufanisi katika sekta ya uwekezaji, tunataka Watanzania wanufaike,”amesema Kairuki

Aidha, amesema kuwa mwaka 2018 mwezi Mei Serikali iliweka mkazo katika andiko la mpango wa kuboresha biashara na uwekezaji pamoja na mpango mkakati wa kuhakikisha kuondoa vikwazo vya biashara mpango ambao unafanikiwa kwa kiwango kikubwa.

Kwa upande wake, Jessica So ambaye ni Mwakilishi wa Balozi wa Heshima wa Tanzania Hongkong amesema kuwa lengo la ujio wao ni kufanya utafiti wa maeneo ya uwekezaji na kibiashara ambapo wanaanza kwa kuangazia maeneo manne yakiwepo ya Sekta ya Dawa, Kilimo cha Ufuta na Korosho pamoja na Sekta ya Utalii.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC, Geoffrey Mwambe amesema kuwa tayari walishafanya mazungumzo na Mamlaka ya maendeleo ya biashara Hongkong ambayo inashughulikia biashara na uwekezaji kusaini makubaliano ya kuhakikisha wafanyabiashara wengi wanatumia fursa zilizopo Hongkong na Tanzania.

 

Wakulima na Wafugaji waliopata majanga waanza kunufaika
Nicki Minaj, Young Money wazitosa tuzo za BET, Sifa kwa Cardi B zachochea