Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema itaendelea kuongeza nguvu katika jitihada za kuzuia na kupambana na ujangili wa wanyamapori na Biashara haramu ya nyara na mazao ya misitu, ili kutokomeza vitendo vinavyoathiri taswira ya nchi, uchumi na maendeleo ya uhifadhi.

Hayo yamebainishwa jijini Arusha Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, John Ngowi ambaye alikuwa alimwakilisha Mkurugenzi Msaidizi wa Uzuiaji Ujangili na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi Taifa cha Kuzuia na Kupambana na Ujangili nchini, Robert Mande.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Msaidizi wa Uzuiaji Ujangili na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi Taifa cha Kuzuia na Kupambana na Ujangili nchini Bw. John Ngowi akiwa kwenye picha ya pamoja na Wenyeviti wa Kamati za Kanda za Kiikolojia za Kuratibu Doria (TCG’s) mara baada ya ufunguzi wa warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa TCG’s.

Ngowi ambaye alikuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Kamati za Kanda za Kiikolojia za Kuratibu Doria (TCG’s), katika kukabiliana na ujangili na Biashara haramu ya wanyamapori nchini amesema Serikali itaendelea kuimarisha mafunzo na doria ili kuhakikisha majangili wanaokamatwa wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Amesema, “Lengo la kutolewa kwa mafunzo haya ni kuharakisha na kuhakikisha majangili wote wanaokamatwa wanafikishwa mahakamani na mashauri yao yanaendeshwa kwa haraka na kwa ufanisi ili wahusika wapewe adhabu inayostahili kulingana na matakwa ya sheria za nchi yetu.”

Mwakilishi wa Mkurugenzi Msaidizi wa Uzuiaji Ujangili na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi Taifa cha Kuzuia na Kupambana na Ujangili nchini Bw. John Ngowi akiwa kwenye picha ya pamoja na Watoa maada kwa  Wenyeviti wa Kamati za Kanda za Kiikolojia za Kuratibu Doria (TCG’s) mara baada ya ufunguzi wa warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa TCG’s.

Aidha ameongeza kuwa, mkakati uliopo katika mapambano dhidi ya ujangili ni kuona watuhumiwa wote wanaokamatwa wanafikishwa mahakamani na mashauri yao yanaendeshwa haraka na kwa ufanisi ili adhabu inayostahili iweze kutolewa kulingana na matakwa ya sheria.

Awali, Meneja wa Mradi wa Kupambana na Ujangili na Usafirshaji haramu wa Nyara, Theotimos Rwegasira amesema mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo Duniani (UNDP) na Shirika la Mazingira (GEF) yatasaidia kupunguza ujangili kwa kiwango kikubwa.

Watendaji Dawati la jinsia waungana kutoa Elimu
Chanjo ya Ebola yawasili baada ya siku 42 bila kesi mpya