Serikali imezindua mwongozo wa Kitaifa wa uanzishaji na uendeshaji majukwaa ya uwezeshaji Wanawake Kiuchumi wenye lengo la kuleta ufanisi wa utekelezaji wa majukwaa haya ikiwa ni pamoja na kuyafanya yajulikane ngazi zote hapa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima ameitaka jamii kuelimisha wanawake juu ya umuhimu wa kujiunga na majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi ili yawawezeshe kupata sehemu ya kujadili mambo yao kuhusu ujasiriamali na biashara kwa ujumla.

Amesema, wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 na mikopo ya Maendeleo ya Wanawake (WDF) inayotolewa na Wizara wahakikishe wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili iwezeshe kuwanufaisha wengine kupata mikopo mapema, na kuzitaka Halmashauri za Wilaya/Manispaa na Majiji ziendelee kutenga fedha za Ndani ili kuwawezesha Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu kukopa na hatimaye kuweza kujiendeleza kiuchumi.

Waziri Gwajima akikabidhi Kitabu cha Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji na Uendeshaji Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa Kaimu Mkuu Mkoa wa Pwani ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri (wa pili kushoto)

Waziri Gwajima, pia ameitaka jamii kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume kushiriki nafasi za uongozi na maamuzi katika ngazi ya jamii na kuwa sehemu ya maamuzi huku akibainisha kuwa “Wanawake na wanaume tuzidi kuungana kupinga ukatili wa kijinsia na kwa watoto kwa kusimamia kurithisha misingi ya maadili mema kwa vizazi vyetu kwani ukatili ni adui wa maendeleo ya kiuchumi.”

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri amesema kuwa kupitia Mwongozo huo Mkoa wa Pwani kupitia Mwongozo huo imeanzisha Kampuni ya Go Mama PLC inayofanya shughuli zake mkoani humo ili kuunganisha wanawake wote kutekeleza shughuli mbali mbali za uwezeshaji wanawake kiuchumi.

Naye, Katibu Mkuu wa ,Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amesema Wizara iliona umuhimu wa kuwa na Mwongozo huu ili kuwa na ufanisi katika ushiriki wao kwenye shughuli za maendeleo zitakazosaidia kuwakwamua kiuchumi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizindua Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji na Uendeshaji Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi uliofanyika Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.

Akitoa salamu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mariam Juma Abdallah amesema Wizara hiyo itasimamia utekelezaji wa Mwongozo huo ili kuwawezesha Wanawake hasa wajasirimali kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli zao mbalimbali.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara (TWCC), Mwajuma Hamza amesema Chama hicho kimefarijika kuona kuwa Serikali imejipanga katika kuhakikisha inawezesha Wanawake hasa katika kuwakwamua kiuchumi kwa kuweka Mwongozo utakaosaidia kuratibu uanzishaji na uendeshaji wa Majukwaa hayo.

Akizungumza katika uzinduzi wa Mwongozo huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Bein’g Issa amesema Baraza lao limeweka mikakati mbalimbali ya kuwezesha wanawake kiuchumi kwa kushirikiana na Wizara ambapo waliratibu uanzishaji wa Majukwaa hayo katika ngazi za Vijiji/ Mitaa, Kata, Wilaya na Mkoa.

Waziri Gwajima (wa kwanza kushoto) akikabidhi Kitabu cha Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji na Uendeshaji Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Pwani, Rachel Chuwa kwa niaba ya Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini.

Ameongeza kuwa, uanzishaji wa Majukwaa umesaidia kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake wajasirimali na jumla ya Majukwaa 26 yameanzishwa katika mikao ya Tanzania Bara, Majukwaa 151 katika Halmashauri, Majukwaa 1,354 ngazi ya Kata na Majukwaa 1,859 katika ngazi ya vijijini/ Mitaa.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 13, 2022  
Tuchel: Nimesikitishwa sana kuondoka Chelsea