Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vya dola viimarishe ulinzi kwenye mipaka ya nchi na hasa katika mwambao wa Bahari ya Hindi ili kuzuia uingizwaji holela wa mchele wa magendo kutoka nje ya nchi.

 

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumatano, Aprili 27, 2016) wakati akijibu hoja za wabunge na kuhitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2016/2017 bungeni mjini Dodoma.

 

“Napenda kuviagiza vyombo vya dola viendelee kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu hasa katika mwambao wa Bahari ya Hindi ili kuzuia uingizwaji holela wa mchele wa magendo kutoka nje ya nchi. Endapo patatokea upungufu wa mchele nchini, Serikali itaangalia uwezekano wa kuruhusu kuagiza mchele kutoka nje,” amesema.

 

Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka sita iliyopita, kumekuwa na ongezeko la asilimia 14 katika uzalishaji wa mpunga hapa nchini na hivyo kufanya kiwango cha uzalishaji kiwe ni kikubwa kuliko mahitaji.

 

Takwimu za uzalishaji mpunga zinaonesha kuwepo ongezeko katika kipindi cha miaka sita iliyopita ambacho kiliongezeka kutoka tani 1,699,825 mwaka 2009/2010 hadi kufikia tani 1,936,909 mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 14. Katika kipindi chote hicho, kiwango cha uzalishaji wa mpunga kimekuwa kikubwa kuliko mahitaji,” amesema.

 

Kutokana na mwenendo huo mzuri wa uzalishaji wa mpunga hapa nchini, Serikali ilisitisha kutoa vibali vya kuagiza mchele kutoka nje ya nchi tangu Machi, 2013. Hatua hii itasaidia wakulima wetu kupata soko la uhakika na bei nzuri, jambo ambalo linawaongezea kipato na pia kuwahamasisha kuongeza uzalishaji zaidi,” amesema.

 

Akizungumzia kuhusu deni la sh. bilioni 134 ambalo Serikali inadaiwa na Bohari ya Dawa nchini (MSD), Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza kulishughulikia deni hilo kwa kumwelekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ahakiki deni hilo. “Mpaka sasa CAG amehakiki madai ya jumla ya shilingi bilioni 67 na kazi ya uhakiki inaendelea.”

 

Akifafanua kuhusu vigezo vilivyutumika kugawanya majimbo mapya ya uchaguzi, Waziri Mkuu alisema mwaka 2015, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea maombi 77 ya kuanzishwa majimbo mapya, ambapo Halmashauri 37 ziliwasilisha maombi ya kugawa majimbo ya uchaguzi na maombi 40 yalitoka katika majimbo yaliyokuwepo yakiomba kugawanywa. Kati ya maombi yaliyowasilishwa, maombi 35 tu ndiyo yalikidhi vigezo na yalistahili kugawanywa.

 

Kutokana na ongezeko la Halmashauri mpya ambazo kisheria ni majimbo ya uchaguzi, ongezeko la idadi ya wabunge wanawake wa viti maalum na uwezo wa ukumbi wa Bunge; Tume iliamua kutumia vigezo vitatu tu ili kupata idadi ya majimbo yanayoweza kugawanywa. Vigezo hivyo ni: Wastani wa idadi ya watu (Population Quota), mipaka ya kiutawala na uwezo wa ukumbi wa Bunge,” alisema.

 

Waziri Mkuu alisema chini ya mchakato huo, Tume ilianzisha majimbo mapya 25 ambapo majimbo 19 yalitokana na ongezeko la Halmashauri mpya; na majimbo sita yalitokana na kigezo cha wastani wa idadi ya watu.

 

Hata hivyo, Waziri Mkuu alibainisha kwamba kwa sasa Serikali haina mpango wa kuongeza maeneo mapya ya utawala zikiwemo wilaya na mikoa mipya kwa sababu bado inaendelea kujengea uwezo wa rasilmali watu na vitendea kazi katika maeneo mapya ya utawala yaliyopo hivi sasa.

Bunge limepitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2016/2017.

Youssoufa Sabo Azibeep Simba, Azam FC Na Young Africans
Boban, Temi Nje City Ikiivaa Mtibwa J’mosi