Meneja wa FC Barcelona, Quique Setien amemaliza tofauti zake na nahodha Lionel Messi na kukubaliana suala la kuiwezesha klabu hiyo kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya msimu huu.

Messi amekuwa akikosoa mbinu za Setien pamoja na wachezaji wenzake, kwamba wamekuwa dhaifu kupita maelezo ndani ya uwanja, hasa baada ya kipigo kutoka kwa Osasuna, ambacho kiliwatibua zaidi na kuwashuhudia wapinzani wao Los Blancos wakitamba na kubeba La Liga.

Lakini, mchezo wao wa mwisho kwenye La Liga, walimaliza kwa staili ya aina yake, waliposhinda 5-0 dhidi ya Alaves Jumapili iliyopita.

Kwa mujibu wa Mundo Deportivo, nguvu ya ushindi huo wa Alaves imekuja baada ya kufanyika kikao baina ya watu wawili wenye nguvu na waliokuwa na tofauti kubwa kwenye kikosi, Messi na kocha wake, Setien.

Bosi huyo wa Nou Camp alikutana ana kwa ana na Messi na kufanya mazungumzo Jumamosi iliyopita, ambapo walimaliza tofauti zao na kuibuka na msimamo mmoja wa kuhakikisha Barcelona inabeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Ripoti zinadai kwamba Setien na Messi walikubaliana kuweka pembeni kutokubaliana kwao kuokoa msimu wa timu hiyo kwa kutimiza ndoto zao katika kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Sote tumepata mzuka mpya kuhusu Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ni jambo la kweli kwamba tumefanya mazungumzo kwa ajili ya kuweka mambo sawa, kwa sababu mambo ni lazima yamalizwe na kuwa sawa,” ilibainisha taarifa kutoka kwa kocha Setien.

FC Barcelona bado wanapewa nafasi kubwa ya kutinga robo fainali kwenye muchuano hiyo wakati watakapowakabili Napoli mwezi ujao, baada ya kufunga bao muhimu la ugenini kwenye sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora iliyopigwa Naples, Italia Februari mwaka huu.

Setien amekuwa kwenye presha kubwa ya kuhusu kibarua chake baada ya bingwa wa La Liga kupatikana kabla ya mchezo wa mwisho wa ligi hiyo, huku ikielezwa mambo yamekuwa hovyo zaidi kwenye vyumba vya kubadilishia huko Nou Camp.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Julai 23, 2020
Sikukuu ya Eid El- Adh'haa kufanyika Ijumaa