Mwanafamilia wa kundi la zamani la ‘Wakilisha’, Shaa amejipanga kuweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza Tanzania kushinda tuzo za muziki zenye heshima kubwa zaidi duniani, Grammy.

Shaa amesema kuwa ndoto yake kubwa ni kuhakikisha anashinda tuzo za Grammy na kwamba baada ya kushinda tuzo hizo ataweza kufikiria kinachofuata kwenye maisha yake kwani atakuwa amefika kilele cha mafanikio.

“Ndoto yangu kubwa sana sana ni kushinda a Grammy. Nikishinda Grammy sijui ndio nitastaafu…sijui lakini nataka kuwa msanii wa kwanza kutoka Tanzania kushinda Grammy,” Shaa aliiambia Lake Fm ya Mwanza.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa ndoto hiyo haimaanishi kuwa hazithamini au hazitaki tuzo za hapa nyumbani, lakini kichwani kwake anaamini tuzo hizo ndizo kipimo cha kujiona umekuwa msanii mkubwa.

Shaa alianza kuonekana kwenye ulimwengu wa muziki aliposhiriki mashindano yaliyoibua kundi la ‘Wakilisha’ akiwa mkali wa kupika vibwagizo na viitikio vya nyimbo kama ‘Swanglish’ na ‘Hoi’, akiwa na marehemu Langa na Witness.

Baadae alijiondoa kwenye kundi hilo na kupata lebo ndani ya MJ Records na sasa ni msanii mkubwa aliyewahi kuweka rekodi kubwa YouTube na wimbo wake ‘Sugua Gaga’.

My Take: Kutoka Sara hadi Shaa… hakuna kinachoshindika, Grammy inawezekana kwani Witness (Wakilisha) aliwahi kuingia kwenye tuzo za Channel O miaka mingi iliyopita wewe unaweza kwenda kokote pia.

Mgandilwa atoa siku tatu kulipwa deni la shil. 270 Kigamboni
Chanzo cha kifo cha rapa Prodigy wa Mobb Deep chawekwa wazi