Na Kika:

Ikitajwa Septemba 11, 2001 wengi tutakuwa tunaikumbuka vyema tarehe hiyo ambayo iliumiza wengi, yalitokea mashambulio manne ya pamoja yaliyofanywa na kikosi cha Kigaidi cha Al-Qaida dhidi ya Marekani.

Ilikuwa kama ‘Script’ ya filamu iliyotekelezwa na kikosi cha Al-Qaida walipoziteka nyala ndege nne wakazitumia kama silaha wakizigongesha katika majengo mjini New York na Washington DC kwa makusudi, kwa mujibu wa taarifa za maofisa.

Katika mashambulio hayo, takribani watu 3,000 walipoteza maisha, wakiwemo watu wa zima moto waliokuwa wakijaribu kuokoa maisha ya baadhi ya watu waliopatwa na balaa hilo na zaidi ya watu 6,000 walijeruhiwa.

Shambulio hilo lilikuwa ndiyo shambulio kubwa la kwanza kwa watu ambao sio Waamerika kushambulia Marekani tangu mwaka wa 1941, pale Wajapani waliposhambulia kituo cha jeshi la maji kilichopo katika Bandari ya Pearl, Hawaii.

Lakini kumekuwa na madai kwamba kuna watu katika Marekani walikuwa wakijua kutatokea tukio kama hilo kabla na ni lini itakuwa hivyo.

Ndege nne zilizotekwa nyala na Al-Qaida ni;  Ndege ya American Airlines Flight 11, iliyotumiwa kugonga mnara wa Kaskazini mwa Jengo la Biashara la Kimataifa (World Trade Center) la mjini New York mnamo saa 8:46:30 asubuhi.

Jengo hilo liliungua kwa muda wa dakika 102 kisha baadaye lilianguka sehemu na mmong’onyoko wa jengo hilo ulipelekea majengo mengine yaliyoyazunguka majengo hayo kushika moto na kuharibika pia.

Lilivyoonekana jengo la Majengo ya Biashara ya Kimataifa (World Trade Center) baada ya shambulio.

Ndege ya United Airlines Flight 175, ilitumiwa kugonga mnara wa Jengo la Biashara la Kimataifa (World Trade Center) la Kusini mnamo saa 9:02:59 asubuhi. Watu wengi waliona tukio la pili kwasababu habari zilikuwa tayari zishasambaa katika mji na kila kamera za televisheni zilikuwa zikielekezea macho yao huko katika eneo la tukio, na wakati huo huo ndege ya pili ikagonga tena mnara wa Kusini mwa Jengo hilo.

Kutokaa na uharibifu uliotokea, jengo la tatu la 7 World Trade Center (7 WTC), nalo likaanguka mnamo saa 5:20 jioni, pia baadhi ya majengo mengine yaliharibiwa vibaya na hata kuangamia kabisa yaani.

American Airlines Flight 77, ilitumiwa kugonga jengo la Pentagon la mjini Arlington, Virginia (karibu kidogo na Washington DC), mnamo saa 9:37:46 asubuhi.

Jengo la Pentagon baada ya kushambuliwa.

Ndege hiyo iligonga chini mwa upande wa Magharibi mwa jengo hilo. Kisha ikagonga mpaka katika nguzo tano zinazoshikiria jengo hilo la Pentagon. Shambulio hilo liliuwa watu 125.

Na ndege ya mwisho, United Airlines Flight 93 hii haikubahatika kugonga mahala popote pale, badala yake wakaiangusha chini mnamo saa 10:03:11 asubuhi.

Iliaminika kwamba magaidi hao walikuwa wakitaka kuigonga ndege ya United Airlines Flight 93 katika jengo la mji mkuu wa Marekani, lakini abiria walijaribu kuinyang’anya ndege hiyo kutoka mikononi mwa magaidi hao lakini hawakufanikiwa, ndipo ndege hiyo ikashia kuanguka karibu na mji wa Shanksville, Pennsylvania.

Eneo la Shanksville, Pennsylvania ilipodondoshwa ndege ya nne ya United Airlines Flight 93 wakati wa mashambulio.

Kilichojiri baada ya mashambulio hayo, Marekani walianza vita dhidi ya ugaidi huku wakiilaumu vikali Al-Qaeda kwa kitendo walicho kifanya.

Kufuatia vita waliyoanzisha Marekani iliyokuwa chini ya Rais George W. Bus , kiongozi wa Al-Qaeda, Osama Bin Laden, akakimbilia nchini Afghanistan.

Bush aliiambia Serikali ya Afghanistan iliyokuwa mkononi mwa kundi la Kiislamu wa Taliban, kumsalimisha Bin Laden mikononi mwao, lakini Wataliban wakagoma na hawakufanya hivyo.

Kiongozi wa Wataliban, Mullah Muhammad Omar, akavimba na kumtaka Bush ampe uthibitisho unaonyesha kwamba Osama anahusika na tukio hilo.

Hapo sasa…! Rais Bush akawa amepandishwa hasira, naye akataka kuonyesha ubabe wake akamwambia Mullah, hapa hakuna haja uthibitisho wowote ule na tangu hapo, Serikali ya Marekani ikaanzisha rasmi vita dhidi ya Afghanistan.

Itaendelea…

#HapoKale imewezeshwa na M-Lipa. Bofya hapo chini kujua zaidi kuhusu M-Lipa

CCM kufanya vikao vya CC, NEC Dar es Salaam
Trump aeleza sababu ya kusitisha ghafla amri ya kuishambulia Iran