Uingereza inaomboleza tukio la kigaidi lililotokea Jumamosi, Juni 20, 2020 baada ya watu watatu kuuawa na wengine kujeruhiwa kwa kuchomwa na visu katika Mji wa Reading nchini humo.

Taarifa zimeeleza kuwa vyombo vya usalama vinamshikilia Khairi Saadallah, raia wa Libya akihusishwa na tukio hilo.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa amewahi kukamatwa na aliachiwa kutoka jela siku 16 zilizopita. Alikamatwa mwaka jana baada ya kubainika kuwa alikuwa anapanga kwenda nchini Syria kujiunga na vikundi vya kigaidi.

Leo, vyombo vya usalama vya Uingereza vimemtaja, Joe Richie-Bennett (35), raia wa Marekani kuwa ni mmoja kati ya waliouawa katika shambulizi hilo. Vimeeleza kuwa alikuwa amekaa katika eneo la Forbury Gardens katika mji wa Reading akiwa na rafiki yake, James Furlong (36), mwalimu wa historia na wote walichomwa visu hadi kufa. Mhanga mwingine aliyepoteza maisha bado hajatajwa jina.

Shuhuda wa tukio hilo, Lawrence Wort ameeleza kuwa alimuona mtu anawachoma watu watatu visu shingoni na kisha akaanza kumfuata yeye akiwa na mpenzi wake. Anasema kuwa walikimbia, ndipo alipohamia kwenye kundi la watu waliokuwa wamekaa karibu.

Balozi wa Marekani nchini Uingereza, Woody Johnson amethibitisha kuwa raia wa Marekani aliuawa katika tukio hilo, akilaani kitendo hicho cha kigaidi.

“Ninatoa salamu zangu za rambirambi kwa familia ya wote waliopoteza maisha. Kwa masikitiko makubwa, hii inahusisha pia raia wa Marekani. Mawazo yetu yako na walioathirika na tukio hili,” amesema Balozi Jonson akikaririwa na Dailymail.

Taarifa ya vyombo vya usalama imeeleza kuwa mtuhumiwa anayeshikiliwa wakati msako wa watuhumiwa mwingine unaendelea, amebainika kuwa ni kijana mwenye umri wa miaka 25 aliyekuwa anakaa karibu nae neo la tukio.

Kijana huyo, Saadallah anadaiwa kuwa alikuwa anapenda kuvuta bangi na kunywa pombe kali, akidaiwa kuwa alikuwa anajitambulisha kwa rafiki zake kama mpiganaji wa kundi la IS. Hata hivyo, ripoti za awali zimeonesha kuwa hakuwa amejiunga moja kwa moja na kundi lolote la kigaidi katika kipindi hiki. Imeelezwa kuwa kijana huyo alikuwa na tatizo la kiakili pia.

Corona: Wakenya wanavyolia na ugumu wa maisha kuliko madhara ya kiafya

Jafo awapa ujumbe mzito walioapishwa leo Ikulu

Simba yatua Mbeya, Bocco aahidi ushindi
Corona: Wakenya wanavyolia na ugumu wa maisha kuliko madhara ya kiafya