Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani vikali ripoti za mashambulizi ya hii leo ya makombora dhidi ya mjiwa bandari wa Odesa nchini Ukraine.

Hayo yamebainishwa katika taarifa iliyotololewa leo Julai 23, 2022 na Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq jijini New York, nchini Marekani.

Shambulizi hilo, limetokea chini ya saa 24 tangu Urusi na Ukraine zitie saini makubaliano ya kuruhusu kuanza kusafirishwa nje ya nchi kwa nafaka na vyakula kutoka Ukraine kupitia bandari Nyeusi.

Mlipuko katika mji wa Odesa nchini Ukraine.

Vyombo vya habari, vinaripoti kuwa makombora mawili yalipiga mji wa Odesa nyakati za alfajiri ya leo Jumamosi Julai 23, licha ya Urusi kupitia makubaliano ya jana ya kukubali kuwa haitolenga bandari wakati shehena za nafaka zikiwa kwenye maandalizi ya kusafirishwa.

Taarifa imemnukuu Katibu Mkuu akisema, ”jana pande zote zilieleza bayana mbele ya dunia nzima kuhakikisha usafirishaji salama wa nafaka na bidhaa nyingine kwenda soko la dunia.”

Guterres amesema bidhaa hizo zinahitajika ili kukabili janga la chakula na kupunguza machungu ya mamilioni ya watu duniani kote wanaohangaika na suala la kupata chakula.

Mlipuko saa chache baada ya makubaliano ya kutoshambulia eneo la Bandari nyeusi.

“Suala la Urusi, Ukraine na Uturuki kutekeleza kwa ukamilifu makubaliano ya jana ni muhimu,” amesema Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres.

Zanzibar kuwa na uchaguzi wa kidemokrasia
Raia 13 wauawa katika mapigano ya wanamgambo