Hatimaye, makubaliano ya kuruhusu meli zilizojaa shehena za nafaka kutoka nchini Ukraine zilizokuwa zimekwama katika mandari za Odessa, Chernomorsk na Yuzhny, kupita kwenye baharí nyeusi yamefikiwa Instanbul Uturuki baina ya Ukraine na Urusi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema, “Makubaliano haya ni nuru ya matumaini, nuru ya unafuu ambao ulimwengu unahitaji kuliko zaidi hivi sasa kuliko hapo awali na ninapenda kuwatambua na kuwashukuru wote waliohusika mpaka kufanikisha hatua hii.”

Amesema, “bila shaka haya ni makubaliano ya ulimwengu na yataleta ahueni kwa nchi zinazoendelea ambazo zipo kwenye makali ya kufilisika na watu walio hatarini zaidi wanaokabiliwa na njaa kali na yatasaidia kuleta utulivu wa bei za vyakula duiani ambazo tayari zilikuwa katika viwango vya rekodi mbaya hata kabla ya vita.

Ramani inayoonesha eneo la Bahari Nyeusi.

Mbali na kuzishukuru nchi hizo mbili, Guterres pia amemshukuru Rais wa Uturuki Recep Erdogan kwa kuwa mwenyeji wa makubaliano hayo ambaye pia nchi yake itakuwa na jukumu la kushirikiana na Umoja wa Mataifa kufanya ukaguzi wa meli hizo za Ukraine ili zisibebe silaha za magendo wakati wa usafirishaji wa nafaka.

Mashirika mengine ya UN yaliyohusika na mchakato huo, ni lile la Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya kibinadamu OCHA na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya kibiashara na maendeleo UNCTAD.

“Nipo hapa kuweka ahadi kamili kuwa Umoja wa Mataifa tutabakia kuwa wahusika wa karibu katika kufanyia kazi na kuhakikisha kuna mafanikio ya makubaliano haya na tutaendelea kuongeza juhudi ili kuhakikisha UN iko katika nafasi nzuri ya kutekeleza ahadi zake,” amesema Guterres.

Meli za wanamaji za Bulgaria na NATO zikishiriki mazoezi ya jeshi la wanamaji la Bulgaria-NATO katika Bahari Nyeusi, mashariki mwa mji mkuu wa Bulgaria Sofia.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo ametangaza kikosi kazi cha kuwezesha utekelezaji wa mpango wa baharí nyeusi kikiongozwa ma Katibu Mkuu wa UNCTAD, Rebecca Grynspan kikijikita katika kuwezesha upatikanaji usiozuiliwa wa chakula na mbolea zinazotoka nchini Urusi kwenda kwenye soko la kimataifa.

Amesema, “Nawaomba pande zote zisiache kipengele chochote na juhudi zozote za utelekezaji wa ahadi zao. Hatupaswi pia kuacha juhudi zozote kwa ajili ya amani, haya ni makubaliano ambayo hayajawahi kutokea kati ya pande mbili zinazohusika katika mzozo wa umwagaji damu.”

Katibu Mkuu, Guterres amehitimisha hotuba yake kwakusema nuru ya matumaini iliyong’aa katika baharí nyeusi ni matokeo chanya ya kuhudi za pamoja za washirika na kuhimiza kuwa nuru hiyo itaangaza njia ya kupunguza mateso yanayowasibu wanadamu na kupatikana kwa amani.

Serikali kufafanua sintofahamu nyongeza ya mishahara
Taarifa ukatili wa kijinsia kusajiliwa rasmi