Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam, Sheikh Ponda Issa Ponda jana alimtembelea mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye yuko mahabusu katika gereza la Kisongo jijini Arusha.

Taarifa za wawili hao kuteta ndani ya gereza hilo zilitolewa na Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Noel Olevarayo.

Olevarayo alieleza kuwa Sheikh Ponda na Lema waliteta kwa muda usiopungua dakika 60 na kwamba Sheikh huyo alimpongeza badala ya kumpa pole kwa kukaa mahabusu kwa muda mrefu.

“Sheikh Ponda amekutana na Mbunge wetu Lema na amekuja mahsusi kumjulia hali,” Alevarayo anakaririwa na Mwananchi.

“Amemuambia hampi pole bali anampongeza kwa kukaa mahabusu muda wote licha ya kuamini anastahili kupata dhamana,” aliongeza.

Lema anaendelea kusota katika mahabusu hiyo baada ya kukwama kufanikisha vigezo vya kisheria kupata dhamana dhidi ya kesi ya uchochezi na kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.

Sheikh Ponda aliwahi kukaa mahabusu kwa muda mrefu akikabliwa na kesi ya uchochezi kabla ya mahakama kutomkuta na hatia na kumuachia huru Novemba mwaka 2015.

Ummy: Vyombo vya habari jiepusheni na habari za uchochezi
Magufuli aanza mchakato wa kuwanyoosha wafuasi wa Lowassa CCM