Kiungo kutoka nchini Sudan Sharaf Eldin Shaiboub Ali Abdelrahman ametambulishwa rasmi kwa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC leo Jumatatu (Januari 03) mchana.

Shiboub ambaye aliwahi kuitumikia Simba SC msimu wa 2019–2020 ameelekea Zanzibar Sanjari na kikosi cha Simba SC na akiwa huko atacheza michezo ya Kombe la Mapinduzi kama kipimo cha kumridhisha Kocha Mkuu Pablo Franco Martin ili amsajili katika Dirisha Dogo.

Kiungo huyo amethibitishwa uwepo wake ndani ya Simba SC sambamba na Kiungo Mshambuliaji kutoka Ivory Coast Moukoro Cheik Tenana ambaye pia atashiriki Michuano ya Mapinduzi.

Simba SC iliyoondoka Dar es salaam majira ya asubuhi, itaanza mchakato wa kulisaka taji la Mapinduzi 2022, keshokutwa Jumatano (Januari 05), kwa kucheza dhidi ya Selem View Uwanja wa Aman.

Simba SC imeelekea Zanzibar ikiwa na kikosi chake kamili, huku Kiungo Mshambuliaji kutoka Malawi Peter Banda akiwa kwenye majukumu ya timu yake ya taifa The Flames inayojiandaa na Fainali za Mataifa ya Afrika 2022 zitakazounguruma nchini Cameroon kuanzia mwishoni mwa juma hili (Januari 09).

Mwaka 2021 Simba SC ilifika Fainali ya Kombe la Mapinduzi na kupoteza kwa changamoto ya Mikwaju ya Penati dhidi ya Young Africans.

Kanye West anaswa akiwa na mwanamke mwingine
Daraja la Wami laelekea kukamilika