Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Njombe imemfikisha katika mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Njombe, Ernest Shauritanga Manga ambaye ni mwenyekiti wa chama cha ushirika cha Kilimani AMCOS kilichopo katika halmashauri ya mji wa Makambako akikabiliwa na kosa la wizi wa sh.milioni tatu(3) ambayo ni mali ya chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari habari ofisini kwake, Kaimu Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Njombe, Charles Mulebya amesema kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu 270 cha sheria ya kanuni ya adhabu (penal code) kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

“Mshtakiwa anadaiwa kuuza kibanda cha biashara mali ya ushirika kwa sh. milioni tisa (9) kwa mfanyabiashara huku akiwasilisha kwenye chama cha msingi milioni sita tu(6) akionyesha ndiyo aliyopokea toka kwa mfanyabiashara huku akijua si kweli,” amesema Kamanda Mulebya

Aidha kamanda huyo wa Takukuru ameongeza kuwa uchunguzi dhidi ya mshatakiwa ulifanyika ili kuthibitisha kosa chini ya sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa na 11/2007,k/f cha 31 kinachohusu matumizi mabaya na madaraka au mamlaka au kutumia madaraka kwa lengo la kujipatia manufaa.

Katika hatua nyingine, Mulebya amesema kuwa baada ya uchunguzi kukamilika na jalada kutolewa maoni ya kisheria, kosa la wizi liliweza kuthibitika bila kuacha shaka yoyote na hivyo kutakiwa kupeleka jalada la uchunguzi katika ofisi ya mashtaka ya Mkoa wa Njombe kwani wanayo mamlaka ya kufungua na kuendesha kesi ambazo makosa yake yapo chini ya sheria ya kanuni ya adhabu.

Hata hivyo, Kamanda Mulebya ameongeza kuwa baada ya ofisi ya Mashtaka kupitia ushahidi uliokusanywa na kuona unatosha kuthibitisha kosa la wizi waliandaa hati ya mashtaka na kesi Na.21/2019 imefunguliwa na mshitakiwa atasomewa maelezo ya awali tarehe 12/2/2019.

Video: STAMICO kutekeleza maagizo ya viongozi katika sekta ya madini
Halmashauri ya Mji Njombe yaipiga msasa Manispaa ya Sumbawanga