Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga mjini  Josephine Matiru ameiomba serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Kujenga kiwanda kitakacho zalisha  mkaa utokanao na mabaki ya miti ambao utakuwa ni rafiki kwa mazingira ili kunusuru hali ya mkoa huo kuendelea kuwa jangwa.

Matiru ametoa ombi hilo leo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,  Luhaga Mpina aliposhiriki siku ya usafi kitaifa ya mwisho wa mwezi Oktoba, ambapo  ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.

Kwa Upande wake Naibu Waziri Mpina amesema kuwa  Serikali iko tayari kujenga kiwanda cha kutengeneza mkaa mjini Shinyanga ili kunusuru hali  hiyo.

“Lazima tuwe na viwanda vya mkaa rafiki kwa mazingira sasa na wafanyabiashara wa gesi za majumbani washushe bei ili asilimia kubwa ya watanzania waweze kutumia nishati hiyo,” alisema Mpina.

Naibu Waziri Mpina Pia ameshiriki zoezi la upandaji miti katika eneoa la Ibinzamata, na kuwataka watanzania  kujijengea utamaduni wa usafi wao pamoja na kutunza  mazingira kwani hata vitabu vitakatifu vinasisitiza usafi wa mazingira, aidha amewataka watendaji katika ngazi zote kuzingatia utekelezaji wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake.

Katika hatua nyngine, Mpina ameagiza kila wilaya na Halmashauri kutengeneza mwongozo na sheria ndogo ndogo katika suala la usafi wa mazingira na upandaji miti ili kuweza kukabiliana na athari zitokanazo na Mabadiliko ya tabia nchi kwa kurudisha uoto wa Asili.

Akizungumzia wananchi wanaoabudu siku ya Jumamosi Mpina amesema Sheria ndogo ndogo za mazingira za Halmashauri na miji ni vizuri wakabuni namna ya kuweza kuwapa nafasi na wao ya kuabudu na kushiriki usafi katika siku hiyo, kila Jumamosi  ya mwisho wa mwezi  imetengwa na serikali maalum kwa ajili ya usafi nchini.

Odinga aituhumu familia ya Rais Kenyatta kwa ufisadi wa mabilioni
Rais Magufuli amtumbua Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai