Siku chache baada ya Rais John Magufuli kutangaza mpango wa kuwapunguzia kiwango cha mshahara watumishi wanaolipwa hadi shilingi milioni 40 kwa mwezi ili wafike milioni 15 kwa mwezi, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limepinga mpango huo.

Naibu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Hezron Kaaya ambaye jana alikuwa akizungumza na viongozi wa vyama vya wafanyakazi jijini Mwanza, amesema kuwa uamuzi huo ni kunyume cha sheria na taratibu na kwamba endapo utatekelezwa kisiasa utaligharimu Serikali iwapo watumishi hao wataamua kwenda Mahakamani kupinga punguzo hilo kwa mujibu wa kikataba kati yao na mwajiri.

Kaaya alisema kuwa Watumishi wanaolipwa mishahara hiyo hawakujipangia wenyewe bali malipo yalipangwa na Bodi ya Mashirika na taasisi zenye Mamlaka hayo kisheria na kwamba mishahara hiyo haiwezi kupunguzwa kwa kauli za kisiasa bila kuzingatia sheria.

“Iwapo Serikali itatekeleza lengo hili bila kuwapo mjadala mpana na makubaliano ya kisheria kati ya wahusika, basi ijiandae kulipa mamilioni ya fedha kama fidia iwapo watakaokatwa mishahara yao watakwenda mahakamani,” alisema.

Alisema kuwa Serikali inapaswa kuendelea kuwalipa mishahara hiyo watumishi hao hadi watakapofikia mwisho wa mikataba yao na kuanza utaratibu mpya wa makubaliano na muajiri au kuwaacha na kuajiri watu wengine.

Bungeni: Wabunge wa CCM, Ukawa wakosoa uamuzi wa Bunge kurudisha Bilioni 6 kwa Magufuli
Chadema - Mbeya wamsusia Mkuu wa Mkoa Amos Makalla, wadai amewapuuza