Beki mahiri wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, amechaguliwa na mashabiki kuwa Mchezaji Bora wa timu hiyo msimu uliopita.

Zoezi la kumtafuta mchezaji wa kutwaa tuzo hiyo lilianza rasmi Juni 8 mwaka huu kwa hatua ya awali kabla ya Ijumaa iliyopita kuingia hatua ya fainali iliyohusisha wachezaji sita waliopigiwa kura nyingi zaidi na mashabiki katika akaunti ya Azam FC kwenye mtandao wa kijamii wa facebook.

Hadi zoezi hilo linakamilika leo Jumatano saa 6.00 mchana, Kapombe amewabwaga wapinzani wake watano kwenye kinyang’anyiro hicho ambao ni Nahodha Msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, beki kisiki Pascal Wawa, kipa Aishi Manula na mawinga Farid Mussa na Ramadhan Singano ‘Messi’.

Beki huyo ametwaa tuzo hiyo baada ya kujizolea kura 203 kati ya zote 560 zilizokubaliwa, Aishi amemfuatia akiwa nazo 125, Farid (95), Singano (48), Himid (45) na Wawa (44).

Jumla ya kura 710 zilipigwa na mashabiki mbalimbali walioshiriki zoezi hilo, lakini ni 560 tu zilizokubaliwa, nyingine 150 ziliharibika baada ya wapigaji kukiuka masharti kwa wengine kupiga kura zaidi ya moja na baadhi yao kuwapigia kura wachezaji wawili tofauti huku zingine zilizokataliwa zikiwa ni kwa wale waliokosea majina.

Mashabiki wengi waliompigia kura Kapombe hawakusita kufanya hivyo wakidai alikuwa ni nguzo muhimu kwa Azam msimu uliopita baada ya kucheza kwa bidii na kufunga mabao muhimu kwa timu hiyo na hata alipokosekana pengo lake lilionekana huku pia wengine wakimpongeza Aishi Manula aliyeshika nafasi ya pili wakisema naye alifanya kazi kubwa.

Mbali na tuzo hiyo ya mashabiki, Kapombe pia alifanikiwa kuwa mchezaji pekee wa Azam FC aliyepata Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi inayotolewa na mdhamini wa Ligi Kuu, Kampuni ya Vodacom, akitwaa ya mwezi Januari mwaka huu.

Moja ya rekodi zake za msimu uliopita, ni kuwa beki pekee wa ligi hiyo aliyefunga mabao mengi kuliko mwingine yoyote akitupia wavuni mabao nane huku katika mechi zote ilizocheza Azam FC akicheka na nyavu mara 12 na kutoa pasi za mwisho saba.

Kapombe aliyecheza jumla ya dakika 3188 msimu uliopita katika mechi zote ilizocheza Azam FC, hakufanikiwa kumaliza vema msimu baada ya miezi miwili iliyopita kuugua ugonjwa wa Pulmonary Embolism (donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu) na kukosa sehemu iliyobakia ya msimu na sasa afya yake inaendelea vema kabisa.

Claudio Ranieri Akata Tamaa, Awafunguliwa Milango Arsenal
Hazard: Sikua Miongoni Mwa Wasaliti Wa Jose Mourinho