Azam FC inaweza kumkosa beki wake wa kulia, Shomary Kapombe katika mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi dhidi ya Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hiyo inafuatia Kapombe kuumia jana katika mchezo wa kimataifa kati ya Tanzania na wenyeji Malawi mjini Blantyre.

Kapombe alimaliza dakika 90 za mchezo huo wa marudiano kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia mwaka 2018 Urusi, lakini akatoka anachechemea.

Baadaye timu iliporejea katika hoteli ya Malawi Sun, Kapombe alikwenda kufanyiwa uchunguzi na Dk Gilbert Kigadye.

Akizungumzia hali ya mchezaji huyo, Dk Kigadye alisema Kapombe anasumbuliwa na maumivu ya nyayo na ni tatizo la muda.

“Imekuwa kawaida yake akicheza kwenye Uwanja mgumu tu, anatoka anaumwa nyayo, ila sitarajii athari kubwa, nadhani hata kesho anaweza kuendelea na mazoezi,”amesema.

Taifa Stars ilifungwa 1-0 na Malawi jana, lakini ikasonga mbele hatua ya mwisho ya mchujo kutokana na ushindi wa 2-0 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam na sasa itamenyana na Algeria mwezi ujao.

Chanzo: Binzubeir

Bado Alama 9, Hamilton Kuwa Bingwa Wa dunia
Magufuli Akabidhiwa 'Faili' La Wasaliti Awashughulikie