Naibu Waziri Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amemfungia Msanii Suzan Michael maarufu kama Pretty Kind kujihusisha na shughuli za Sanaa kwa muda wa miezi sita.

Naibu Waziri Shonza amechukua hatua hiyo leo jijini Dar es Salaam kutokana na msanii huyo Kutoa wimbo usiyo na maadili wenye jina la ‘’Viduduwasha’’, Kufanya kazi ya Sanaa bila kusajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa, pamoja na kuweka mtandaoni picha ya nusu utupu kinyume na maadili ya Kitanzania.

‘’Kumekuwa na wimbi kubwa la wasanii sasa hivi kutoa nyimbo zenye maneno ya matusi na zisizo na maadili pamoja na wasanii hasa wanawake kupiga picha wakiwa wamevaa nusu utupu na kuweka picha hizo katika mitandao,nataka kuwapa angalizo wasanii wenye tabia hizi kuwa Serikali inawafuatilia kwa karibu na mwaka huu tumeanza na huyu na wengine wanafuata kama msanii Gift Stanford maarufu kama Gigy Money na  Jane Rimoy maarufu kama Sanchi,’’ Shonza.

Shonza ametoa msisitizo wa kumtaka msanii Gigy Money kufika ofisini kwake haraka, kutokana kuwa hivi karibuni alimtumia ujumbe wakumtaka afike ofisini kwake lakini bado hajafika mpaka sasa hivyo amemwambia kuwa atambue hawezi kushindana na Serikali.

Kwa upande wa Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Godfrey Mngereza  katika mkutano huo alieleza kuwa kwa mujibu wa Kanuni  31(1) ya Baraza ya mwaka 2005,inaeleza kuwa msanii kufanya kazi bila kusajiliwa ni kosa na anaweza kufungiwa, na pia kwa upande wa mavazi zinasema msanii anatakiwa kuvaa mavazi yenye stara yasiyomdhalilisha wala kudhalilisha watazamaji wake.

‘’Napenda kuwasisitiwa wasanii wote ambao wanajijua kuwa hawajasajiliwa BASATA kuja kujisajili haraka na kwa wale waandaji wa kazi za Sanaa kama waongozaji wa (Directors), Waandaaji (Producers) na wamiliki wa Studio za kurekodi kazi za Sanaa  ambao hawajasajiliwa nao waje kujisajili haraka’’ Mngereza.

Pamoja na hayo naye Msanii Suzan Michael Maarufu kama Pretty Kind aliomba radhi mashabiki wake kwa kufanya makosa hayo pamoja na watanzania wote kwa ujumla na kuaahidi kujirekebisha na kuto kurudia tena makosa hayo.

Halikadhalika Naibu Waziri Shonza ametoa rai kwa wamiliki wa vyombo vya Habari kutokubali kupiga nyimbo au video za nimbo zisizo na maadili kwani  wanakuwa ni sehemu ya kutangaza vitendo hivyo vilivyo kinyume na maadili  kwani itafika mahali serikali itachukulia hatua hata vyombo vinavyopiga nyimbo zisizo na maadili.

Magazeti ya Tanzania leo Januari 8, 2018
Majaliwa awaweka kitimoto Mawaziri