Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amewataka waandishi wa habari nchini kuzingatia maadili kwa kuandika habari zenye ukweli na uhakika kwa manufaa ya Taifa na Watanzania kwa ujumla.

Ameyasema hayo hii leo katika maadhimisho ya siku ya Redio Duniani, ambapo kitaifa yamefanyika mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na waandishi na watangazaji wa redio za jamii kutoka mikoa ya Arusha, Iringa, Morogoro, Mtwara, Shinyanga, Songwe, Geita, Mwanza, Kagera, Dodoma, Pemba, Unguja, Lindi na Songwe.

“Redio za jamii zimekuwa tegemeo kubwa la kupata habari kwa wananchi wa maeneo mbalimbali hapa nchini hasa pembezoni mwa nchi. Mwananchi hahitaji kuwa na umeme anapotaka kusikiliza Redio,”amesema Shonza.

Amesema kuwa ni vyema waandishi wawe wakweli wanapotoa habari mbalimbali kwa wananchi ili kuepuka machafuko ya nchi kama ilivyotokea nchini Rwanda, ambapo chanzo cha machafuko hayo kilitokana na habari zilizotangazwa kupitia Redio.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge amewata waandishi wa habari kuitangaza Dodoma pamoja na fursa zilizomo mkoani humo kwa kuwa ni ya Serikali ni kuifanya Dodoma kuwa kituo cha mji wa kiuchumi.

Hata hivyo, Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Faith Shayo amewataka waandishi wa habari hao kutumia vizuri vipaza sauti vyao katika kudumisha amani ya nchi, kuchochea maendeleo, kupinga unyanyasaji wa kijinsia pamoja na kuweka msisitizo wa  usawa wa kijinsia.

Dkt. Mwakyembe ayafunda mashirikisho ya Sanaa na Filamu
Kenyatta ashangazwa na kitendo cha mwanasheria mkuu kujiuzulu