Taasisi ya Tumaini Fund mkoani Kagera imetoa msaada kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu na kukabidhi madawati 30 vyote vikiwa na thamani ya Sh. 76 milioni kwa shule ya Msingi Kihinga wilayani Ngara ailiyoathiriwa na bomu Novemba 2017 na kusababisha wanafunzi watano kufariki na wengine 43 kujeruhiwa.

Mratibu wa taasisi hiyo, Alex Nyamkara akiambatana na Mwenyekiti wa mfuko huo Dkt. Suzan Wilson kutoka nchini Uingereza wamekabidhi miundombinu hiyo kwa shule hiyo baada ya tukio la bomu lililoharibu madarasa manne

Amesema kuwa wakati wa tukio taasisi hiyo ilitoa msaada wa matibabu yaliyogharimu Sh. 6 milioni kwa wanafunzi waliojeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Misheni Rulenge wilayani Ngara.

“Msaada mwingine ni wanafunzi wa shule nzima walipewa vifaa vya darasani majeruhi walipatiwa sare za shule na vifaa vya kujifunzia na familia zilizopoteza watoto zilipewa pole ya vyakula kama kuwafariji,” amesema Nyamkara

Aidha, kwa upande wake Dkt. Suzan amesema kuwa wanafunzi watatu waliopata ulemavu wa kudumu atarudi hapa nchini kuwaletea vifaa maalumu vya kutumia kulingana na ulemavu wao ili kuweza kuendelea na masomo yao.

Wanafunzi waliopata ulemavu wa kudumu ni Emanuel Hilali, Melania Razalo, ambapo walipofuka macho na kuwekewa macho ya bandia katika Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro na Domina Wabandi aliyebaki na uoni hafifu.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Ngara Luteni Kanali, Michael Mtenjele ameitaka jamii ya shule hiyo kutunza miundombinu iliyotolewa na taasisi ya Tumaini Fund na kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama katika kijiji hicho.

3.5 Bilioni kujenga makazi ya Askari Polisi
Huwezi kuwaita Wabunge wa CCM 'Makasuku'- Lusinde