Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amewachapa viboko wanafunzi watano waliohusika katika tukio la kuchoma moto shule ya sekondari ya Wavulana ya Oswe na kusababisha hasara ya Zaidi ya Tsh. Milioni 26.

RC Mwangela amefikia hatua hiyo mara baada ya kamati aliyoiunda ya kuchunguza chanzo cha ajali ya moto uliotokea shuleni hapo Julai 3 mwaka huu kubaini kuwa wanafunzi wawili Naftari Nganga na Collin Kisinga ndio waliochoma mabweni ya shule hiyo huku wenzao watatu wakiwa na taarifa za mipango hiyo na hawakuripoti.

Kufuatia tukio hilo, ametoa miezi mitatu kwa Wazazi wa Naftari na Collin kila mmoja alipe shilingi Nilioni 7.3, Mmiliki wa Shule pia alibainika kuwa na uzembe wa kuweka vifaa vya kuzimia moto hivyo ameagizwa alipie Tsh. Milioni 7.3 huku Mwalimu wa zamu siku ya tukio, mlinzi na Patroni nao wakitakiwa kulipa Tsh. Milioni 4 ili kufidia hasara iliyotokana na ajali hiyo ya moto.

Amesema wanafunzi hao walianza mpango wa kuchoma moto mabweni June 28 kwa kununua vifaa vya kuchomea, ilipofika Julai 2 walijaribu kuchoma bweni lakini halikuwaka, July 3 walichoma bweni likawaka na kusababisha hasara hiyo na July 6 walifanya jaribio lingine tena la kuchoma moto ghala la chakula lakini halikuwaka moto.

Aidha Brig. Jen Mwangela  amewaagiza maafisa elimu wote Mkoa wa Songwe kuhakikisha wanafanya ukaguzi katika shule zote ili kubaini endapo elimu ya tahadhari ya majanga ya moto na vifaa muhimu kwa ajili ya kuzima moto vimewekwa katika maeneo ya shule pamoja na kuzingatia taratibu na miongozo ya uendeshaji wa shule.

Pia amewataka wanafunzi kuzingatia masomo na kuacha tabia za kujiingiza katika vitendo viovu vinavyoweza kuharibu maisha yao kwani taifa linawategemea wawe wananchi bora na viongozi au watendaji wa baadae.

Rais Magufuli ameahirisha sherehe za Mashujaa
Trump ‘apiga chini’ sheria ya kuvaa barakoa