Shule ya Wasichana ya Starehe nchini Kenya imefungwa kwa dharura baada ya kuzuka ugonjwa usioeleweka uliosababisha wanafunzi 52 walioathirika kutengwa.

Mkurugenzi wa Elimu wa Mkoa wa Nairobi, Jared Obiero amesema kuwa wamelazimika kuifunga shule hiyo ili kuepuka kusambaa kwa ugonjwa huo. Obiero amesema wanatarajia kuifungua tena shule hiyo Jumatatu ijayo, Oktoba 7, 2019.

Wanafunzi wanaougua ugonjwa huo wameonesha dalili mbalimbali zikiwemo kukohoa wakitoa mlio wenye sauti kali ya kubana, kupiga chafya na homa ya kiwango cha chini, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa shule hiyo.

Timu ya madaktari ilifika katika shule hiyo na kukusanya sampuli ambayo imewasilishwa Taasisi ya Utafiti wa Tiba Kenya (KEMRI).

Matokeo ya utafiti huo yalipaswa kuwekwa wazi leo, lakini uongozi wa shule hiyo umesema kuwa bado hawajawasiliana na wazazi wa wanafunzi. Wameeleza kuwa baada ya kuwasiliana na wazazi wote ndipo watatoa taarifa kwa umma.

Kwa mujibu wa The Citizen, maafisa kutoka Wizara ya Afya na madaktari kadhaa wa kujitolea wapo katika shule hiyo wakiangalia hali inavyoendelea.

Mganga wa kienyeji ashtakiwa kwa kumbaka mtoto wa miaka nane
AU yaipa Tanzania ujumbe kuhusu ulinzi wa amani duniani