Nchini Uganda hatimaye siku ya leo wanafunzi wamefanikiwa kurudi shuleni tangu kusitishwa masomo kwa muda mrefu zaidi duniani.

Serikali ya Rais Yoweri Museveni iliamuru mamilioni ya wanafunzi kurudi shuleni takriban miaka miwili baada ya kusimamishwa kwa shughuli za masomo nchini humo kwa sababu ya janga la UVIKO-19

Wanafunzi wapatao milioni 15 hawajahudhuria shule nchini Uganda tangu Machi 2020 wakati madarasa yalipofungwa huku Corona ikienea zaidi ulimwenguni. 

Waziri wa Elimu John Muyingo alisema wanafunzi wote watarejelea masomo mwaka mmoja juu ya kiwango walichokuwa kabla ya shule kufungwa.  

“Shule zote zimetekeleza miongozo na taratibu za kawaida za uendeshaji ili kuhakikisha watoto wanarudi salama shuleni, na hatua zimewekwa kuhakikisha wale ambao hawatatii wanafanya hivyo,” aliiambia shirika la habari la AFP.

Muyingo alisema shule zote za kibinafsi hazitakiwi kudai ada zaidi ya viwango vya kabla ya janga.

Mashirika ya kutetea haki za watoto yamekosoa uamuzi wa Uganda wa kufunga shule kikamilifu au kwa sehemu kwa muda wa wiki 83, muda mrefu zaidi kuliko mahali pengine popote duniani.

 “Hatuwezi kuruhusu hili kutokea tena. Ni lazima tuweke shule wazi kwa kila mtoto, kila mahali,” shirika la Umoja wa Mataifa la kutetea haki za watoto UNICEF lilisema kwenye Twitter. 

Kwa upande wao, wazazi wameelezea furaha yao kwamba angalau sasa watoto watakuwa katika mazingira ambayo ni salama kwao kuliko kubaki mitaani kwani wengi wamejiingiza katika vitendo viovu  ikiwemo wengine kushiriki ukahaba na kupata mimba. Kero nyingine kwa wazazi ni bei ghali ya vifaa vya matumizi shuleni.

Kulingana na ratiba iliyotokewa na serikali, wanafunzi wa viwango mbalimbali watarudi shuleni kwa makundi ili kuepusha misongamano na hii leo ni wanafunzi wa vidato vya tano na sita ndiyo wametakiwa kurudi pamoja na wale  katika shule za kutwa.

Shirika la hisani la Save the Children lilisema wanafunzi wangetatizika kubadilika baada ya kuwa nyumbani sana, na kuonya kuwa kunaweza kuwa na viwango vya juu vya kuacha shule katika wiki zijazo pasipokuwa na uingiliaji wa haraka wa kusaidia wanafunzi. 

Dereva na Kondakta wanashikiliwa kwa kumshambulia 'Trafiki'
Dkt. Tulia achukua fomu za U-Spika