Maandalizi ya uchaguzi wa urais nchini Zimbabwe yameongeza kasi ya ushindani wa kisiasa huku mdahalo wa wagombea urais wawili wenye nguvu ukizua mijadala.

Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amekataa kushiriki mdahalo kati yake na mpinzani wake mkuu, Nelson Chamisa ikiwa ni sehemu ya mbio za uchaguzi utakaofanyika mwaka huu.

Kwa mujibu wa NewsDay, msemaji wa Rais huyo atakayepeperusha bendera ya Zanu-PF, George Charamba amesema kuwa rais haoni umuhimu wa kushiriki mdahalo huo utakaorushwa moja kwa moja na vituo vya runinga kwani anazo njia nyingi zaidi za kuwafikia wananchi.

Charamba amesema kuwa Mnangagwa anaona kushiriki mdahalo huo ni kama kuuza mbinu zake za kampeni mapema kwa mpinzani wake, hivyo atatumia njia nyingine za kuwafikia wananchi wengi kwa muda mfupi na kuwaomba kura.

“Sidhani kama tunataka mdahalo wa wagombea urais hata kidogo kwa sababu hatuoni kama una thamani yoyote. Moja kati ya njia muhimu ya kuwasiliana katika siasa ni kwenda moja kwa moja kwa wapiga kura. Na hatuoni kama mdahalo utatufikisha huko,” alisema Charamba.

Chamisa amekuwa akimtaka Mnangagwa kushiriki mdahalo huo akidai kuwa endapo atakuli, ataanika mambo mengi ya rais huyo yanayoonesha kukosa shukurani.

Zimbabwe inatarajia kufanya uchaguzi wa kwanza wa urais bila jina la Robert Mugabe, tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru Aprili 18, 1980.

Jumia yazidi kuwasogezea huduma bora wananchi, yaleta kampeni ya 'Big Home Makeover'
Salamba mchezaji bora mwezi Machi