Kapteni Samwel Balina Gibuyi ambaye ni rubani wa ndege 5H –WXO inayomilikiwa na Shirika la PAMS Foundation inadaiwa amepotea tangu tarehe 18 Oktoba na mpaka sasa hajaonekana pamoja na ndege aliyokua akiiongoza.


Gibuyi anaongoza ndege ya shirika hilo ambalo hufanya kazi na Shirika la Uhifadhi wa Wanyama katika Hifadhi ya Jumuiya ya Nalika iliyopo Kijiji cha Matemanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.


Kwa mujibu wa taarifa rubani huyo alipotea akiwa na ndege ndogo ambayo hutumika na shirika hilo kwa ajili ya doria na kufukuzia wanyama wakali ambao wamekuwa wakivamia makazi ya wananchi pamoja na kuharibu mashamba ya wakulima katika maeneo hayo.


Oscer Bubambezi ambaye ni Meneja wa Mradi wa PAMS Foundation Ukanda wa Kusini amesema kuwa, Kapteni Gibuyi aliruka na ndege hiyo Oktoba 18, mwaka huu katika Kituo cha Kiuma wilayani Tunduru majira ya saa 09:09 alasiri akiwa katika Hifadhi ya Pori la Selous Kingupira wilayani Rufiji mkoani Pwani.


Bubambezi amesema, baada ya tukio hilo kwa bahati mbaya Kapteni Gibuyi hakufika katika kituo alichokuwa amekusudia kwenda na hajarudi hadi leo hali inayowatia mashaka kwa shirika pamoja ma wafanyakazi wenzake na kuwafanya waripoti katika Mamlaka ya Anga Tanzania kwa usaidizi na wao kuanzisha doria za ardhini na angani ili kumtafuta katika pori hilo bila mafanikio.


Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Tunduru, Limbega Hasan amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba Serikali inatoa ushirikianao wa hali na mali katika kufanikisha zoezi la kupatikana kwa rubani huyo.


Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mheshimiwa Julius Mtatiro amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba juhudi za kuitafuta ndege hiyo pamoja na rubani huyo zinaendelea kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kupitia ndege tano zinazopita angani, magari, pikipiki na watu wanaotembea kwa miguu katika pori hilo

Rais Samia kuelekea Scotland
Marufuku kufunga ving'ora gari binasfi