Viongozi wa dini Tanzania wametangaza kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa muda wa siku saba nchi nzima ili aendelee na juhudi zake za kulinda raslimali za watanzania kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya dini zote, Askofu William Mwamalanga kwa niaba ya viongozi wa dini leo jijini Dar es Salaam.

“Tumeamua kufanya maombi ya siku saba kwa kumtaka kila mtanzania popote alipo kutembea hatua saba kila siku akimwombea Mhe. Rais Magufuli ili Mungu amlinde pamoja na anaofanyanao kazi kwa usahihi (uaminifu)”, alisema Askofu Mwamalanga.

Askofu Mwamalanga amesema kuwa maombi hayo yataanza kesho Juni 15 nchi nzima na yatajumuisha watu wa dini zote nchini, yaani madhehebu ya Kiislam, Kikristo, Kihindu, Budha na madhehebu mengine, ambapo ndani ya siku hizo kila mtanzania atakuwa ametembea jumla ya hatua 49 akimwombea Rais Magufuli na wezalendo wenzake.

Viongozi hao wa dini wamepanga kumpongeza Rais Magufuli mara baada ya kuchukua hatua madhubuti za kutaka waliohusika kwa namna yoyote kuiba raslimali za Taifa hususani madini, wanachukuliwa hatua na kuitaka kampuni ya ACCASIA kulipa kile ambacho walichukua kinyume cha sheria.

Aidha, Askofu Mwamalanga amesema kuwa Kamati yake inamwomba Rais Magufuli achukue hatua za haraka kudhibiti raslimali za nchi kwa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambako mali nyingi zinatoroshwa na wajanja wachache.

Pia, amemwomba Rais Magufuli aziunganishe Wizara za Nishati na Madini na Maliasili na Utalii na kuunda wizara moja ambayo itasimamia kwa karibu raslimali za watanzania.

“Tunamwomba Rais Magufuli amchague mtu makini na mzalendo mwenye uchungu na nchi hii ili asimamie wizara hiyo, na nina hakika wizara hiyo ikisimamiwa vizuri, ndoto ya Rais ya kuifanya Tanzania kuwa nchi mhisani itatimia kwa kuwa hapa Mungu ametujalia kila kitu”,alisema Askofu Mwamalanga.

 

Wanafunzi shule za msingi wagoma, wafunga barabara ya jiji
?Breakingnews: Rais Magufuli akutana na Barrick, Acacia wakubali kulipa fedha wanazodaiwa