Ukoma ni mojawapo ya magonjwa ya kihistoria duniani ambao umekuwepo tangu enzi na enzi.Hadi mwaka 2008 ukoma uliaminika kuwa unasababishwa na aina moja tu ya bakteria ambao ni Mycobacterium leprae ambapo aina ya pili ya bakteria jamii ya M.lepromatosis walipogunduliwa nchini Mexico kuwa na uwezo wa kusababisha ukoma.Nchi za India,Brazil na Indonesia ndizo hubeba zaidi ya 80% ya wagonjwa wote duniani.

Tofauti na jinsi inavyoaminika,ukoma siyo ugonjwa wa laana wala kurogwa na hauambukizwi kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine ikiwa mgonjwa ataanza kutumia dawa mapema.Kila mtu anaweza kuugua ugonjwa huu wakati wowote,mahali popote,hivyo unyanyapaa na kuwatenga watu wenye tatizo hili siyo sawa na tunapaswa kuacha kushikilia mila hizi potofu kabisa.
Njia kubwa sana ya kusambaa kwa ugonjwa huu ni kupitia majimaji yanayozalishwa na pua (nasal droplets and secretions) pia kupitia hewa. Kushirikiana au hata kugusana na watu wenye tatizo hili hakuna uhusiano wowote na kusambazwa kwake , Ukoma huathiri sana ngozi,mfumo wa fahamu pamoja na viungo vya mwili hasa miguu,mikono,pua,macho,figo pamoja na kusababisha ugumba na utasa kwa wanaume walio na ukoma Lepromatous leprosy.

Katika taarifa yake Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto Ummy Mwalimu ameeleza kuwa Siku hii inatupa fursa ya kutathmini mwelekeo wa jitihada zetu nchini na za kimataifa katika kupambana na ugonjwa huu. Kauli mbiu ya mwaka 2020 ni Tuthamini Haki, Utu wa Waathirika wa Ukoma kwa kutokomeza Ubaguzi, Unyanyapaa, na Chuki.

Unyanyapaa na Ubaguzi dhidi ya waathirika wa Ukoma huwafanya watu wajifiche na kushindwa kujitokeza katika vituo vya huduma kwa ajili ya matibabu na hivyo kupelekea kupata ulemavu wa kudumu. Mbaya zaidi kuchelewa kwa wagonjwa hawa kupata matibabu ni chanzo cha mwendelezo wa maambukizi mapya katika jamii.

“Ninatoa wito kwa jamii, wadau na wananchi wote kuuungana na Serikali ili kuongeza nguvu ya kupinga matukio yote ya Ubaguzi na Unyanyapaa dhidi ya waathirika wa ukoma. Hatua hii itatusaidia kupiga hatua katika kutokomeza ukoma nchini”

“Hali ya Ukoma Tanzania tayari imefikia viwango vya kidunia vya kutokomeza ukoma vya kuwa chini ya wagonjwa 10 kati ya watu 100,000 mnamo mwaka 2006. Kwa mwaka 2019, idadi ya waathirika wa ukoma nchini ni wagonjwa 3 katika kila watu 100,000” ameeleza Waziri Mwalimu

 Na kuongeza kuwa “Hata hivyo tunazo Halmashauri 16 ambazo bado hazijafikia viwango hivyo. Hizi ni Manispaa ya Lindi, Liwale, Nachingwea, Ruangwa, Masasi, Nanyumbu, Morogoro, Mvomero, Mpanda, Nkasi, Manispaa ya Shinyanga, Manispaa ya Kigoma, Kibaha, Mkinga na Tunduru”
Aidha ametoa agizo kuwa “Ninazitaka Halmashauri hizi kuongeza kasi ya kutokomeza Ukoma na kuhakikisha kaya zote hatarishi na zenye wagonjwa wa ukoma zinafikiwa, wanakaya wanachunguzwa na wale ambao tayari wanaugua wanatibiwa kikamilifu”
Dalili za Ukoma ni pamoja na baka au mabaka yenye rangi ya shaba mwilini ambayo hayaumi wala hayawashi. Tujichunguze ngozi mwili mzima kila wakati. Ukiona dalili nenda kituo cha Huduma kwa uchunguzi, Ushauri na Tiba.

Maziwa mtindi kinga dhidi ya mafua
Video: Maswali tata kung'olewa Kangi Lugola