Rais wa klabu ya AC Milan, Silvio Berlusconi amekata mzizi wa fitna kuhusu mustakabali wa mshambuliaji kutoka nchini Italia, Mario Balotelli aliyekua akiitumikia klabu hiyo kwa mkopo.

Berlusconi ambaye anatambulika kwama mtu mwenye msimamo katika maamuzi, ametangaza rasmi kutohitaji kumuona mshambuliaji huyo kikosini mwake msimu ujao wa ligi kutokana na kiwango chake kutoridhisha.

Rais huyo amesema Balotelli, atarejeshwa kwenye klabu yake ya Liverpool, kutokana na kutoona sababu zozote za kuendelea kubaki San Siro, kama ilivyokua ikielezwa hapo awali, ambapo baadhi ya vyombo vya habari viliwahi kuripoti huenda mshambuliaji huyo angesajiliwa moja kwa moja.

“Mkataba wa mkopo kati yetu na Balotelli, umeshamalizika na hatujaridhishwa na kiwango chake, hivyo hatuna namna ya kuendelea kubaki nae hapa zaidi ya kurudishwa Liverpool,” Alisema Berlusconi alipokua akizungumza na mwandishi wa tovuti ya Telelombardia.

Katika hatua nyingine kiongozi huyo ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa Italia amethibitisha kuondoka kwa wachezaji wengine klabuni hapo katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa ligi.

Amesema wameshamalizana kimkataba na Alex, Philippe Mexes pamoja na Kevin-Prince Boateng.

“Dhamira yetu ni kutaka kuona tunakijenga upya kikosi chatu kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, tunamshukuru kila mmoja ambaye hatokua nasi, na ninaamini bado kuna nafasi ya kuendelea kucheza soka kwa upande wao.” Aliongeza Berlusconi.

Balotelli, mwenye umri wa miaka 25, hakuwa na msimu mzuri tangu alipojiunga na AC Milan kwa mkopo na mpaka sasa anathibitishiwa kuondoka mjini Milan, amefanikiwa kufunga bao moja.

Goal Line Technology Kutumika Copa America 2016
Video: 'Hii michezo haitaki hasira' - Abdallah Ulega