Wakati dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufungwa leo Ijumaa (Januari 15) mishale ya saa tano na dakika hamsini na tisa usiku, Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wanatajwa kufanikisha mpango wa kumsajili mshambuliaji Perfect Chikwende kutoka FC Platinum ya Zimbabwe.

Mshambuliaji huyo ambaye aliifungua bao pekee FC Platinum kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza dhidi ya Simba SC mjini Harare, Zimbabwe, alikua anahusishwa na mpango wa kusajiliwa na Azam FC, hivyo taarifa za kuwa mikononi mwa mabingwa wa Tanzania Bara zinafuta mpango huo.

Hata hivyo kocha mkuu wa Azam FC George Lwandamina anatajwa kuwa kizuizi cha kusitishwa kwa dili la usajili wa Chikwende huko Azam Complex Chamazi, baada ya kujiridhisha hana mashiko kwenye mipango yake ya ufundi.

Kama tetesi za usajili wa Chikwende zitakua kweli, Simba watakua wamefanya usajili wa wachezaji wawili katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, baada ya kuanza na Thadeo Lwanga ambaye ni kiungo mkabaji.

Lwanga alikuwa kwenye kikosi cha Simba ambacho kimeshiriki Kombe la Mapinduzi na alicheza pia kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Young Africans, ambao ulimalizika kwa mabingwa hao kupoteza kwa changamoto ya mikwaju ya Penati 4-3.

Maalim Seif ameokoa ndoa za watu
Museveni aongoza matokeo ya awali