Uongozi wa klabu ya simba, umesisitiza kuzitumia vyema fedha za malipo ya ada ya usajili wa aliyekua mshambuliaji wao kutoka nchini Uganda, Emmanuel Arnold Okwi kwa ajili ya ujenzi wa uwanja.

Simba imepata uhakika wa kulipwa fedha hizo kutoka kwenye klabu ya Etoile Du Sahel ya nchini Tunisia ambayo ilimsajili mshambuliaji huyo mwaka 2013, kwa ada ya usajili wa dola za kimarekani 300,000.

Kauli hiyo ya Simba imetolewa na msemaji wake Haji Manara,ambaye amesema taarifa walizonazo ni kwamba tayari pesa hiyo kiasi cha dola laki tatu kimeshaingia kwenye akaunti yao na kinachosubiriwa kwa sasa ni kamati ya utendaji kuidhinisha matumizi yake.

Simba inayoongoza ligi kwa wakati huu imekuwa ikidai pesa hiyo kwa muda mrefu kiasi cha shirikisho la soka duniani kuingilia kati na kutoa agizo kwa klabu ya Etoile hadi kufikia mwezi huu wa machi iwe imeshalipa deni vinginevyo rungu kali la kisheria lingewaangukia.

Tangu kuzaliwa kwake miaka 80 iliyopita,Simba haijawahi kuwa na uwanja wake licha ya kubadilisha viongozi mara kwa mara kwa mujibu wa katiba lakini kila kiongozi ajaye huishia kupiga porojo za ujenzi wa uwanja na kutoa ahadi zisizotekelezeka.

Hili litakuwa ni jambo la kihistoria endapo Simba itatekeleza kwa vitendo kipaumbele chake hicho cha ujenzi wa uwanja kwa kutumia pesa za Okwi,na kuufanya uongozi wa rais Evans Aveva kuwa wa mfano wa kuigwa kuwahi kutokea.

Tanesco yamnyooshea mikono Magufuli, yatangaza haya
Miraj Adam Kuwakosa Simba Kesho Mkwakwani