Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, wamepanga kuondoka nchini Jumapili (April 4) kuelekea Cairo Misri, kwa ajili ya mchezo wa mwisho hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya mabingwa watetezi Al Ahly utakaochezwa April 09.

Simba SC imepanga kuondoka na wachezjai 25 muda mfupi baada ya mchezo wao dhidi ya AS Vita Club, utakaochezwa kesho Jumamosi (Appril 03) Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam kuanzia saa kumi jioni kwa saa za Afrika mashariki.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez amesema msafara wa kikosi cha Simba utapitia Dubai, kisha kuelekea mjini Cairo Misri, ambapo utakaa mjini humo kwa siku kadhaa kabla ya mchezo wake dhidi ya Al Ahly.

“Baada ya mchezo wetu wa kesho Jumamosi dhidi ya AS Vita Club, Jumapili timu itasafiri kuelekea Cairo kupitia Dubai tayari kwa ajili ya mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Al Ahly.

“Benchi la ufundi limependekeza kikosi kitakachoenda Misri kiwe na wachezaji 25 lakini pia kwenye msafara kutakuwa na viongozi na waandishi wa habari,” amesema Barbara.

Simba SC inaongoza msimamo wa Kundi A kwa kufikisha alama 10, ikifuatiwa na Al Ahly yenye alama 7, AS Vita inashika nafasi ya tatu kwa kumiliki alama 4 na AlMerrikh wanaburuza mkia kwa kupata alama moja kwenye michezo minne waliocheza.

Wananchi walalamikia gharama za mitandao kupaa
Waziri Ummy: TAMISEMI sio ngumu