Wachezaji wa klabu ya Simba ambao hawakuitwa kwenye vikosi vya timu zao za taifa kwa ajili ya michuano ya kombe la Challenge, wanatarajiwa kurejea mazoezi mwanzoni mwa juma lijalo, kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mchezo wa mzunguuko wa 12 wa ligi kuu ya soka Tanzania bara.

Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Simba zinaeleza kuwa, wachezaji wamepewa siku saba za mapumzika kutokana na Ligi Kuu ya soka Tanzania bara kusimama kwa muda, kupisha michuano ya kombe la Challenge itakayoanza mwishoni mwa juma hili nchini Kenya.

Kikosi cha Simba kimepewa mapumziko ya siku saba, huku kikiendelea kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara kikiwa na pointi 23 baada ya kucheza michezo 11.

Meneja wa Simba, Richard Robert amesema kwa sasa wametoa mapumziko kwa wachezaji wote ambao hawakuitwa kwenye timu zao za taifa, ili watakaporejea waanze kazi rasmi kujiandaa na michezo ijayo ya ligi kuu pamoja na kombe la Mapinduzi.

Katika michuano ya kombe la Mapinduzi itakayoanza kuunguruma kisiwani Unguja mwishoni mwa mwezi ujao, Simba watafungua michuano hiyo kwa kucheza dhidi ya URA kutoka nchini Uganda Januari mbili 2018.

Simba imepangwa Kundi A pamoja na Azam FC, Jamhuri, Taifa ya Jang’ombe na URA ya Uganda, wakati Young Africans imetupwa Kundi B pamoja na JKU, Mlandege, Zimamoto na Shaba.

Simba itamenyana na Azam FC Januari 6, ikitoka kukipiga na Taifa ya Jang’ombe Januari 4, kabla ya kumalizia michezo yake ya Kundi A Januari 8 dhidi ya Jamhuri.

Tiketi 742,760 za kombe la dunia zauzwa
Manara autamani Urais