Bodi ya Wakurugenzi Simba Sc imeanza mkakati maalum wa usajili ili kukiboresha kikosi chao kupitia Dirisha Dogo la usajili ambalo linatarajiwa kufunguliwa siku za usoni.

Simba SC siku za karibuni imekua ikionesha mchezo usiovutia licha ya kupata matokeo yanayoipa alama tatu, hali ambayo imewaibua baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo na kuutaka Uongozi kufanya usajili kupitia Dirisha Dogo, ambalo wanaamini utaleta mabadiliko kwenye kikosi chao.

Simba SC imekuwa ikipewa sapoti kubwa kutoka kwa Rais wao wa Heshima Mohamed Dewji ‘Mo’ ambaye amekuwa akishiriki kwenye mambo ya usajili, imepanga kufanya vyema katika hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, mara baada ya misimu kadhaa kuishia hatua ya Robo Fainali.

Taarifa ambazo tumezipata kutoka kwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC ambaye hakutana jina lake kuanikwa hadharani zinaeleza kuwa, Uongozi umepangwa kufanya usajili wa kisasa kwa kutumia Mawakala kutoka Barani Ulaya na Afrika Magharibi kuhakikisha wanapata wachezaji wenye uwezo mkubwa zaidi ya waliopo kikosini kwa sasa.

“Kama Uongozi tukiri kuwa usajili wa msimu huu kuna baadhi ya nafasi tumeshindwa kuzifanyia usajili baada ya kuwakosa wale wachezaji tuliokuwa tunawahitaji.”

“Hivyo basi tumepanga kuja kivingine katika usajili wetu, ni kuwapa kazi hiyo wataalamu ambao ni Mawakala kutoka Barani Ulaya na Afrika Magharibi.”

“Kikubwa tunahitaji kusajili Mshambuliaji mmoja ambaye ni Mshambuliaji halisi namba 9, kwani hivi sasa tunamtumia Moses Phiri, ambaye kiasili ni namba 10.”

“Pia tumepanga kumsajili Kiungo Mshambuliaji na Mchezeshaji wote wenye viwango vya juu watakaotuvusha kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.” amesema Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC

Hadi sasa Simba SC ina nafasi moja ya kusajili mchezaji Kimataifa, iliyoachwa wazi na Mshambuliaji kutoka nchini Serbia Dejan Georgijević aliyeamua kuvunja mkataba na klabu hiyo miezi miwili iliyopita.

Pia kuna tetesi zinazoeleza kuwa baadhi ya wachezaji wengine wa Kigeni huenda wakatemwa wakati wa Dirisha Dogo la Usajili ili kupisha usajili wa wachezaji wapya klabuni hapo.

Injinia Hersi atuma ujumbe mzito CAF
HAT TRICK yampa jeuri Mayele, afunguka mazito aliyopitia