Tanzania ina nafasi kubwa ya kupeleka timu nne kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao, kufuatia kufanya vizuri kwa klabu ya Simba SC kwenye michuano ya klabu Bingwa Barani Afrika, huku Namungo FC ikitanguliza mguu moja kwenye hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Tayari Simba SC imeshaanza michezo ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na imeshinda mchezo mmoja dhidi ya AS Vita Club, huku Namungo FC ikivuna ushindi wa mabao 6-2 dhidi ya Clube Desportivo 1º de Agosto ya Angola kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya 32 Bora.

Mchongo wa Tanzania kupeleka timu nne kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao upo hivi: Kabla ya kuanza kwa msimu huu wa mashindano ya CAF, Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 13 katika viwango vya ubora wa soka barani Afrika Afrika upande wa vilabu, ikiwa na alama 14.

Alama (Point) hupatikana kwa klabu kuingia hatua ya makundi. Kwa Ligi ya Mabingwa, kuingia tu makundi, nchi inapata alama 2.5, Shirikisho ni alama 2.

alama hizi huhesabiwa kwa kipindi cha miaka 5 na mwaka wa karibu zaidi huwa na thamani zaidi. Kila unapopita mwaka mmoja, alama moja hupungua kwa kila alama za mwaka husika.

Tanzania tulizipata alama zetu kwa mafanikio ya Young Africans (2016 na 2018) na Simba SC (2018/19).

Young Africans waliingia makundi Shirikisho na kuipatia Tanzania alama 2 kila mwaka. Lakini hadi kufikia 2018/19 pale Simba SC walipoingia robo fainali, pointi za Young Africans zilipungua na kubaki 3.

Robo fainali ya Simba SC iliipatia Tanzania alama 15, ukichanganya na zile 3 za Young Africans, zikawa 18…tukapanda hadi nafasi ya 12 Afrika na kuingiza timu 4 kwenye mashindano ya CAF.

Lakini kukwama kwetu misimu iliyofuata kulitupunguzia alama. Hadi msimu huu unaanza tukabaki na alama 14 tu ambazo msimu ujao zitabaki 13.

Lakini Simba kuingia makundi kumetupatia alama 2 ambazo zinafanya tuwe na alama 15 msimu ujao.

Hata hivyo, kwenye ligi ya mabingwa, kuingia makundi kuna alama zake na kila nafasi utakayomaliza kwenye kundi ina alama zake.

Nafasi ya mwisho ina alama 5…kwa hiyo Simba SC hata akiwa wa mwisho kwenye kundi, Tanzania itavuna alama 5, ukijumlisha na zile 13, zitakuwa 18 msimu ujao.

Wapinzani wetu wakubwa nchi ya Libya, ambao walianza msimu wakiwa na alama 16.5, zitapungua hadi kuwa 13.5 msimu ujao.

Lakini kwa kuwa timu yao ya Al Ahly Benghazi imeingia hatua ya makundi Kombe la Shirikisho, msimu ujao Libya itakuwa na alama 15.5, bado hawatotufikia.

Na endapo Namungo FC wataingia hatua ya makundi, wataipatia Tanzania alama 2, na zile 18, zitakuwa alama 20.

Ili Libya watuzidi, ni lazima kwanza timu zetu zote ziishie makundi halafu yao ifike hadi robo fainali.

Manara: Siitanii tena Young Africans
Aliyekuwa Gavana Benki kuu afariki dunia