Klabu ya Simba SC imethibitisha kumuuza Kiungo Mshambuliaji kutoka nhini Zambia Rally Bwalya leo Ijumaa jioni (Juni 16), baada ya kufikiwa kwa makubaliano rasmi kati ya pande hizo mbili.

Simba SC kupitia Simba APP imethibitisha taarifa hizo kwa kuwafahamisha Mashabiki na Wanachama wake, ambao katika kipindi hiki wamekua karibu na vyanzo vya habari vya klabu hiyo, ili kufahamu nani anasajiliwa na nani anaondoka klabuni hapo.

Taarifa ya Simba SC imeeleza: “Uongozi wa klabu yetu umefikia makubaliano ya kumuuza  Kiungo Mshambuliaji Rally Bwalya kwa timu ambayo hatutaiweka wazi kwa sasa, kutokana na matakwa ya kimkataba.”

Bwalya aliyesajiliwa Simba SC msimu wa 2020/21 akitokea Pawer Dynamo ya nchini kwao Zambia ataondoka klabuni hapo mwishoni mwa mwezi huu, huku tetesi zikieleza kuwa huenda akajiunga na klabu ya Amazulu ya Afrika Kusini.

Akiwa Simba SC kiungo huyo alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa Ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ msimu wa 2020/21.

Pia alitwaa Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimu uliopita kwa kuichapa Namungo FC mabao 2-0 jijini Arusha, pamoja na Kombe la Mapinduzi mwaka huu 2022.

Upande wa kimataifa Kiungo huyo alikua sehemu ya kikosi cha Simba kilichofika Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu uliopita (2020/21), na msimu huu 2021/22 alikuwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo kilichotinga hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Mzozo wa Rwanda na DRC wazidi kufukuta
Ukraine yalalamikia uharibifu wa makombora ya Urusi