Mashabiki na Wanachama wa Simba SC wameombwa kuwa wastahamilivu katika suala la kuatangazwa kwa Kocha Mkuu mpya wa klabu hiyo, ambaye atarithishwa mikoba ya Sven Vandenbroeck.

Simba wametoa ombi hilo kwa mashabiki na wanachama wao, kupitia mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Ijumaa (Januari 22), jijini Dar es salaam.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliokua unasubiriwa kwa hamu na wadau wa soka nchini kote, Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Barbara Gonzale, amesema suala la kocha litawekwa hadharani siku kadhaa zijalo.

Barbara, akatumia mkutano huo kutangaza michuano SIMBA INTER CUP ambayo itashirikisha timu tatu, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, itakayoanza mwezi ujao.

Amesema timu tatu zitakazoshiriki michuano hiyo ni Simba SC, TP Mazembe ya DR Congo na Al Hilal ya Sudan. Michuano hiyo imepangwa kuanza Januari 27 hadi 31, 2021 jijini Dar es salaam.

“Kabla ya mashindano kuanza tutakuwa tumeshamtangaza kocha mpya hivyo kesho mashabiki watamjua kocho mpya wa Simba wasiwe na mashaka,” amesema Barbara.

Ikumbukwe Vandebroeck ambaye alikua kocha mkuu wa klabu hiyo aliachana na Simba SC baada ya kufanikiwa kuivusha timu na kuingia kwenye hatua ya makundi katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika.

Tetesi za usajili barani Ulaya
Tanzania, Congo wapigwa marufuku kuingia Uingereza