Kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC kimeondoka jijini Dar es salaam kuelekea kisiwani Unguja (Zanzibar), tayari kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani humo.

Simba SC imeondoka leo mchana kuelekea Unguja (Zanzibar), baada ya kukamilisha mpango wa kuitoa FC Platinum kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kwa kuifunga mabao manne kwa sifuri katika mchezo wa mkondo wa pili uliochezwa jana Jumatano (Januari 06) Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Simba SC imesonga mbele kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao manne kwa moja, na sasa inasubiri kupangwa kwa droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2020/21.

Dakika chache kabla ya kuanz safari ya kuelekea Unguja (Zanzibar), Simba SC kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii waliandika ujumbe mzito, ambao umechukuliwa kwama dongo kwa wapinzani kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu 2021.

Ujumbe ulioandikwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za klabu hiyo unasomeka: “Kwenye shughuli akiingia mgeni rasmi ndio uzinduzi unafanyika rasmi. Wengine ulikuwa utangulizi wanaume ndio tunaenda kuanza kazi kwenye MapinduziCup.”

Simba SC itaanza kampeni ya kusaka ubingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa kucheza dhidi ya Chipukizi FC kesho Ijumaa (Januari 08) saa kumi jioni, wakifuatiwa na watani zao wa jadi Young Africans ambao watawakabili Namungo FC mishale ya saa mbili usiku.

Simba SC imepangwa kundi B na mabingwa watetezi Mtibwa Sugar na Chipukizi FC, huku Young Africans walioshindwa kufurukuta kwenye mchezo wao wa kwanza kwa kulazimishwa sare ya bila kufungana, wamepangwa kundi A na Jamhuri FC na Namungo FC.

Azam FC ipo kundi C sambamba na Mlandege FC na Malindi FC.

Wanne wafariki baada ya wafuasi wa Trump kuvamia bunge
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Januari 7, 2021