Uongozi wa klabu bingwa Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba, umekanusha taarifa za kuondoka kwa kocha Patrick Aussems bila ya ruhusa.

Gazeti la Mwana Spoti, leo limeripoti kuwa kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji jana jumatatu alionekana uwanja wa ndege akiondoka nchini, bila ya taarifa maalum kutoka kwa viongozi wa Simba SC.

Afisa amtendaji mkuu wa Simba SC Senzo Mazingiza, amesema ana taarifa za kuondoka kwa kocha Aussems, japo hakumueleza ni wapi alipoelekea kwa ajili ya kutatua dharura inayomkabili.

Hata hivyo amesema kocha Aussems atakaporejea ataviarifu vyombo vya habari kuhusu kurejea kwake, ili kuondoa mkangnyiko uliojitokeza, na kuwachanganya mashabiki na wanachama wa Simba SC.

“Kocha Aussems bado ni muajiriwa wa klabu ya Simba. Alinitumia barua pepe jana Jumatatu akiniarifu kuhusu dharura aliyoipata, hivyo amesafiri japo hakusema ni wapi alipoelekea, atakaporejea nitatoa taarifa.” Amesema Senzo Mazingiza.

Kocha aussems ameondoka huku kikosi chake kikikabiliwa na mchezo wa kirafiki, ambao utachezwa leo usiku kwenye uwanja wa Azam Copmplex Chamazi, dhidi ya maafande wa jeshi la kujenga taifa (JKT Tanzania).

Kwa mantiki hiyo kocha msaidizi Denis Kitambi, anatarajiwa kukiongoza kikosi cha Simba kama mkuu wa benchi la ufundi, katika mchezo huo wa kirafiki.

Mwishoni mwa juma lililopita kikosi cha Simba kilifungwa na KMC FC mabao mawili kwa moja, katika mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Simba SC inaendelea kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Ruvu Shooting ambao utaunguruma mwishoni mwa juma hili, Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es salaam.

Mkwasa kufumua mfumo wa Mwinyi Zahera Young Africans
Etienne Ndayiragije: Tutapambana bila Erasto Nyoni