Baada ya kuivusha Simba SC kutoka hatua ya awali hadi Mzunguuko wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuwabanjua Mabingwa wa Malawi ‘Nyasa Big Bullet’, Kocha Mkuu wa muda wa wababe hao wa Msimbazi Juma Ramadhan Mgunda amefunguka kuhusu mipango ya kuivaa Primero de Agosto ya Angola.

Simba SC ilitinga hatua ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-0, wakishinda mabao mawili katika michezo ya nyumbani na ugenini, huku de Agosto waliibanjua Red Arrows ya Zambia jumla ya mabao mawili kwa moja, wakishinda ugenini 1-0, kisha wakilazimishwa sare ya 1-1 nyumbani.

Kocha Mgunda amesema hatua inayofuata kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni ngumu na ina changamoto zake, hivyo hana budi kupambana kwa ajili ya kubuni mbinu ambazo zitakisaidia kikosi chake kufanya vizuri mbele ya de Agosto ya Angola.

Amesema timu hiyo ni nzuri na kubwa katika ukanda wa Bara la Afrika, lakini wameanza kuifuatilia kwa kuangalia baadhi ya michezo waliyocheza siku za karibuni, ili kubaini sehemu ya mbinu zao.

“Unajua kila unapovuka hatua moja kwenda nyingine kayika michuano hii ya Afrika, changamoto ya upinzani inazidi kuwa kubwa, wapinzani wetu ni wazuri na tuna kila sababu ya kujihadhari nao kwa sababu haya ni mpambano, hatuna budi kusaka mbinu za kushinda vita,”

“de Agosto ni timu kubwa tunaendelea kuwafuatilia kwa kuangalia baadhi ya Michezo yao waliocheza siku za karibuni ili kuangalia uimara wao uko wapi ili tuone jinsi gani tutaenda kupambana nao.”

“Baada ya kuamaliza mchezo wetu dhidi ya Nyasa Big Bullet, vijana wamepewa mapumziko ya siku mbili baada ya hapo watarudi kambini kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.” amesema Mgunda.

Simba SC itaanzia ugenini dhidi ya Primero de Agosto kati ya Oktoba 7-9 kisha itarejea nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kwa mchezo wa Mkondo wa pili utakaopigwa kati ya Oktoba 14-16.

Al Hilal yamuumiza kichwa Nassredine Nabi
STAMICO na GST kutafiti madini Kilombero na Mufindi