Uongozi wa Simba SC umesema unasubiri Ripoti ya Kaimu Kocha Mkuu Juma Ramadhan Mgunda, ili kuanza Mpango wa kukamilisha usajili wa Wachezaji watakaopendekezwa kupitia Dirisha Dogo.

Simba SC imeshathibitisha kufanya usajili wakati wa Dirisha Dogo, ambalo rasmi litafunguliwa Desemba 16 na kufungwa Januari 15 mwaka 2023.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema pamoja na na kujipanga kusajili wamekua wakisikia taarifa za kuhusishwa na usajili wa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibanzonkiza.

Ahmed amesema Mchezaji huyo ni mzuri na bado ana mkataba na klabu nyingine, hivyo kama atapendekezwa kupitia Ripoti ya Kocha Mgunda watafanya jitihada za kumsajili.

“Saido bila shaka ni mchezaji mzuri mwenye uzoefu na kiwango bora na nakumbuka sababu iliyomfanya aondoke upande wa pili (Young Africans), ni kutokana na masuala ya nidhamu.”

“Tunasubiri ripoti ya usajili kutoka kwa Kocha wetu Juma Mgunda na tukiona Saido anafaa kucheza Simba SC, basi tutawasiliana na Uongozi wa Geita Gold FC na kufanya taratibu za kumsajili.” amesema Ahmed Ally

Simba SC imemaliza Duru la Kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23, ikiwa nafasi ya tatu katika Msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha alama 34, huku Azam FC na Young Africans zikifikisha alama 35.

Fei Toto awaahidi mazito mashabiki Young Africans
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Decemba 7, 2022