Wekundu wa Msimbazi Simba wamedhihirisha dhana yao ya kutaka ubingwa msimu huu, baada ya kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa kuichapa Singida Utd mabao manne kwa sifuri katika mchezo wa mzunguuko wa 13.

Kabla ya mchezo huo Simba walikua katika nafasi ya pili, kutokana na matokeo ya sare ya bao moja kwa moja yaliyopatikana mjini Songea kati ya Azam FC na Majimaji FC, ambapo Azam FC walifikisha point 27 na kuwaacha Wekundu hao wakiwa na point 26.

Mabao yaliyofungwa na mshambuliaji kutoka nchini Uganda Emmanuel Arnord Okwi, Asante KWasi na Shiza Ramadhan Kichuya yalitosha kuipa heshima nyingine Simba ya kurejea kileleni kwa kufikisha point 29.

Mchezo huo uliochezeshwa na refa Jacob Adongo wa Mara, aliyesaidiwa na Mohammed Mkono wa Tanga na Gasper Ketto wa Arusha hadi mapumziko Simba SC walikuwa wanaongoza kwa mabao mawili kwa sifuri.

Kiungo Shiza Ramadhani Kichuya alianza kuifungia Simba SC dakika ya tatu akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo mkongwe Mwinyi Kazimoto, kufuatia John Raphael Bocco kuangushwa nje kidogo ya boksi.

Singida wakacharuka na kuanza kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Simba kusaka bao la kusawazisha, lakini ngome ya Wekundu wa Msimbazi ikiongozwa na Erasto Edward Nyoni ilikuwa imara kuondosha hatari zote.

Beki Mghana, Asante Kwasi akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 25 akimvisha kanzu kipa Peter Manyika aliyetoka langoni bila hesabu nzuri baada ya pasi ndefu ya kiungo Said Ndemla aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Kazimoto.

Bao hilo lilionekana kuwachanganya Singida United wanaofundishwa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm na kuwaruhusu Simba kutawala zaidi mchezo huo.

Okwi akatokea benchi dakika ya 65 kuchukua nafasi ya kiungo Muzamil Yassin na akafunga mabao mawili ndani ya dakika saba.

Alifunga bao la tatu dakika ya 75 akimalizia pasi ya Shiza Kichuya na la nne dakika ya 82 akimalizia pasi ya Ndemla. Alifunga mabao hayo, baada ya kumsetia pasi nzuri Kichuya, akapiga nje akiwa ndani ya sita.

Video: Makamu wa Rais akagua mifereji Jijini Dar
Mtambue kocha mpya wa Simba SC