Kikosi cha Simba SC kimerejea jijini Dar es salaam kikitokea mjini Bukoba mkoani Kagera kilipokua na mchezo wa ‘KIPORO’ wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar.

Simba SC ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa 1-0 jana Jumatano (Januari 26), katika Uwanja wa Kaitaba na kuwafanya Mabingwa hao watetezi kufikisha michezo miwili waliyopoteza msimu huu 2021/22.

Simba SC imeendelea kubaki nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 25, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 35, huku Kagera Sugar ikishika nafasi ya tisa kwa kufikisha alama 16.

Kwa mujibu wa kurasa rasmi za Mitandao ya Kijamii za Simba SC, kikosi cha Simba SC kimerejea jijini Dar es salaam kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania).

Simba SC itarejea tena dimbani Jumapili (Januari 30) kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Dar City katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Filamu ya Bongo yawaogopesha Wakenya
Harmonize aitangaza siku yake