Wenyeji wa mchezo wa WATANI WA JADI Simba SC, wametangaza viingilio vya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa Mashabiki wa soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.

Simba SC inayotetea Ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22, itaikaribisha Young Africans Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi (Desemba 11), huku ikiwa na lengo la kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wa Ngao ya Jamii.

Simba SC ilipoteza kwa 1-0 dhidi ya Young Africans mwezi Septemba, huku bao pekee la Wananchi likifungwa na Mshambuliaji wao kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele.

Simba SC imetangaza viingilio vya mchezo huo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, ikiwa ni desturi ya klabu hiyo kufanya hivyo katika kila mchezo wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ama michuano ya Kimataifa.

Kiingilio cha chini katika mchezo huo wa Desemba 11 kitakua Shilingi 5,000 huku kiingilio cha juu kimetajwa kuwa Shilingi 30,000.

Tayari Young Africans imeshaanza maandalizi ya mchezo huo, huku Simba SC ikitarajia kuanza kambi mara itakaporejea Dar es salaam, ikitokea Lusaka-Zambia ilipokua inakabiliwa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Mkondo wa Pili hatua ya Mtoano dhidi ya Red Arrows.

Mchezo huo uliochezwa jana Jumapili (Desemba 05), Simba SC ilipoteza kwa kufungwa 2-1, lakini imefuzu hatua ya Makundi kwa ushindi wa jumla wa 4-2.

Mwakalebela aichimba MKWARA Simba SC
Chama cha FDP chaidhinisha makubaliano ya serikali ya muungano