Aliyekua Kiungo Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Nicholas Gyan amesema hana imani kama klabu yake ya zamani itaweza kutetea Ubingwa wa Ligi msimu huu 2021/22.

Gyan ambaye kwa sasa anaitumikia klabu ya DTB inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, amesema kuanza vibaya kwa Simba SC na kuendelea kwa msigano ndani ya klabu hiyo kwa sasa kunampa shaka, kama watafanikiwa kuendelea kuwa na furaha ya ubingwa.

Kiungo huyo kutoka nchini Ghana, hakusita kuelekeza mawazo yake ya Ubingwa msimu huu, kwa kuutaja upande wa pili (Young Africans) kwa kusema una kikosi imara na madhubuti ambacho kinamuaminisha kitaweza kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne.

“Uwa natazama mechi ya Simba na Young Africans kama ambavyo imekuwa desturi ya Watanzania wengi. Young africans wanaonekana kuwa wanahitaji kitu msimu huu.”

“Na kwa namna ambavyo walivyo bora naona wanakwenda kufanya mambo makubwa sana, siyo Young Africans ile ya misimu minne nyuma, hii iko bora zaidi na Simba wanatakiwa kuwa makini zaidi kwa kuwa mwisho wanaweza kutoka kapa.”

Young Africans inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 9, ikitanguliwa na Polisi Tanzania yenye alama 9, huku Simba SC iliyocheza michezo miwili hadi sasa ikiwa na alama 4 zinazoiweka kwenye nafasi ya 9.

Simba SC leo Jumatano (Oktoba 27) itacheza mchezo wake wa tatu dhidi ya Polisi Tanzania, jijini Dar es salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Fei Toto: Sitachoka kuibeba Young Africans
Magori: Wapuuzeni wenye nia ovu