Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC kimewasili salama jijini Cairo, Misri kikitokea Dubai kilipokuwa kimeweka mapumziko ya muda tangu jana Jumanne (April 06), baada ya kuwasili kikitokea jijini Dar es salam.

Msafara wa Simba SC wenye watu 55 ikiwa ni pamoja na wachezaji, benchi la ufundi pamoja na viongozi, umewasili Cairo, Misri kuwafuata wapinzani wao Al Ahly kwa ajili ya kumaliza mchezo wao wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Baranbi Afrika hatua ya Makundi.

Tayari Simba SC imeshakata tiketi ya kucheza hatua ya Robo Fainali ikiongoza msimamo wa ‘Kundi A’ baada ya kukusanya alama 13, ikifuatiwa na Al Ahly ambayo pia imeshajihakikishia kucheza hatua hiyo kwa kufikisha alama 8, huku AS Vita Club ya DR Congo yenye alama 4 na Al Merrikh yenye alama 2 zikiondoshwa kwenye michuano hiyo.

Mchezo kati ya Al Ahly dhidi ya Simba SC unatarajiwa kuchezwa Ijumaa (Aprili 9) nchini Misri, huku wenyeji wakikumbukia kichapo cha bao 1-0 walichokipata jijini Dar es salaam mwezi Februari.

Bao pekee na la ushindi la Simba SC lilifungwa na mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Msumbiji Luis Miquissone kwa pasi ya Clatous Chama na wote wapo kwenye msafara wa kuelekea jijini Cairo,Misri.

Wengine ambao wapo kwenye msafara wa Simba kwa upande wa wachezaji ni pamoja na Meddie Kagere, Bernard Morrison, Said Ndemla, Ibrahim Ajibu, John Bocco na Larry Bwalya.

Kevin de Bruyne asaini upya Man City
TPA yadhamiria kuvunja rekodi ukusanyaji mapato