Msimu mpya wa 2022/23 umepangwa kuanza rasmi Agosti 13, kwa mchezo wa Ngao ya Jamii kuchezwa katika Uwanja utakaotajwa na Mamlaka za soka nchini Tanzania.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ‘TPLB’ Almas Kassongo leo Jumanne (Juni 28) amezungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam, na kuweka wazi kalenda ya matukio kwa msimu mpya 2022/23, ambayo imeshehemi tarehe za michezo ya Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na Michuano ya Kimataifa.

Rasmi mchezoya Ligi Kuu Tanzania Bara imepangwa kuanza kuunguruma katika viwanja tofauti siku nne baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii (Agosti 17).

Upande wa Michezo ya Kimataifa kalenda hiyo ya Matukio kwa msimu ujao imeainisha michezo ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika, sambamba na michezo ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika ‘AFCON 2023’.

Kalenda hiyo inaonyesha msimu wa 2022/23 utafikia tamati Juni 10 kwa michezo ya mtoano (Play Off) kuchezwa kwa timu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza (Championship).

Wakati huo huo Kasongo ametoa ufafanuzi wa mchezo wa Ngao ya Jamii kwa kusema, kikanuni mchezo huo hukutanisha Bingwa wa Ligi na Bingwa wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, lakini iwapo Bingwa wa Ligi na ‘ASFC’ akiwa ni mmoja, basi mchezo huo utawakutanisha mshindi wa Ligi Kuu na aliyemaliza nafasi ya pili kwenye msimamo.

Hadi sasa Young Afrika Africans imeshatawazwa kuwa Mabingwa wa Ligi Kuu, Simba SC imejihakikishia nafasi ya pili, kwani alama zake haziwezi kufikia na klabu inayoshika nafasi ya tatu na kuendelea.

Hivyo kuna dalili za miamba hiyo kukutana tena katika mchezo wa Ngao ya Jamii, endapo Young Africans itashinda mchezo wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ dhidi ya Coastal Union mjini Arusha mwishoni mwa juma hili (Julao 02).

Sabasaba 2022 kampuni za nje zaongeza ushiriki
Wakimbizi 46 wafariki ndani ya lori