Kutokana na agizo la Waziri mwenye dhamana ya michezo, Nape Nnauye, siku chache zilizopita  kupiga marufuku timu za Simba na Yanga kutumia Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kwa siku zisizojulikana, Simba wako kwenye hatua za mwisho kupeleka maombi yao Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutumia Uwanja wa Azam Complex, ulioko Chamazi kama uwanja wao wa nyumbani.

Hatua ya Simba kuhamishia mechi zao kwenye Uwanja wa Chamazi imetokana na uharibifu mkubwa wa uvunjifu wa viti majukwaani pamoja na mageti ya nje ya uwanja siku ya mchezo kati ya Simba na Yanga maarufu ‘Kariakoo Derby’, mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo Serikali iliamua kuzuia mgawo wao wa pesa za viingilio hadi pale watakapobaini gharama za matengenezo yake.

Licha ya Ofisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara kuwa na kigugumizi cha jambo hilo na kusema atalitolea ufafanuzi leo kwenye vyombo vya habari, lakini taarifa za ndani zinadai kuwa, Simba wanakimbilia Uwanja wa Azam Complex ili kuepuka gharama.

“Tupo kwenye kikao taarifa rasmi za klabu kuhusu uwanja wetu wa nyumbani utakuwa wapi, timu itaweka wapi kambi na mambo mengine kwa ujumla tutaweka wazi kesho (leo),” alisema Manara.

Hata hivyo, makundi mbalimbali ya wapenzi na mashabiki wa Simba yameonyesha kuunga mkono wazo la kuipeleka timu Chamazi kwani ni karibu na wapenzi wao wengi ambao watapata fursa ya kuiona timu yao kuliko kuipeleka mikoani.

Simba wanaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 17, baada ya kushuka dimbani mara saba na kuwapita watani zao Yanga kwa pointi sita zinazowaweka katika nafasi ya tano licha ya kuwa na faida ya mchezo mmoja wa kiporo dhidi ya JKT Ruvu.

Wekundu hao wa Msimbazi watavaana na Prisons ya Mbeya katika mechi ijayo baada ya wiki mbili zijazo kutokana na baadhi ya mechi kusimama kwa muda wikiendi hii kufuatia wachezaji wake kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania(Taifa Stars).

Video: Wafanyabiashara Dodoma watakiwa kuboresha biashara zao
Mkakati Wa Ukodishaji Waiva, Bodi Ya Wadhamini Yaweka Mguu Sawa