Katika kuhakikisha inarejesha makali yake, uongozi wa Simba umemsainisha kocha wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Hemed Suleiman Morocco ambaye anakuja ‘ku-boost’ benchi la ufundi linaloongozwa na Mganda, Jackson Mayanja.

Morocco amefundisha klabu mbalimbali hapa nchini zikiwemo Coastal Union, JKT Oljoro na Zanzibar Heroes iliyo chini ya nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga. Morocco pia ni Kocha Msaidizi wa Taifa Stars.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Kamati ya Utendaji ya Simba, zimesema Morocco anakuja kuwa mshauri mkuu wa benchi la ufundi ambako ameanguka saini ya miezi sita.

Chanzo makini kimeeleza anatarajiwa kuanza kazi leo Jumatatu.

Alipofuatwa Morocco na kuuliza taarifa za kuanguka saini Msimbazi akakiri kuwa ni kweli na muda wowote anatarajia kuanza kibarua baada ya kufikia makubaliano mazuri na uongozi wa Simba.

Lakini akashindwa kubainisha kama atabwaga manyanga kuinoa Stars akidai wanaendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kujua hatima yake baada ya kupata ulaji mpya.

“Wakati wowote natarajia kuanza kazi, baada ya kufikia makubaliano mazuri na viongozi wa Simba,” alisema Morocco.

Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Simba, Enock Kiguha, alikiri kuwa wamemalizana na kocha huyo lakini akadai suala la muda wa mkataba linabaki kuwa siri ya klabu.

“Tumeingia mkataba na Morocco. Ataanza majukumu yake muda si mrefu,” alisema

Mhariri wa Gazeti la Mawio Azungumzia Kufutwa kwa gazeti lake
Tundu Lissu adai Dk. Slaa amepata majibu aliyouliza kuhusu Lowassa