Wekundu Wa Msimbazi Simba wameendelea kulisogelea taji la ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu wa 2017/18, baada ya kuichabanga Mbeya City mabao matatu kwa moja Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Dakika 90 za mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi kutoka mjini Tanga Hance Mabena akisaidiwa na Jesse Erasmo wa Morogoro na Rashid Zongo wa Iringa, zilishuhudia Simba wakipata mabao hayo kupitia kwa mshambuliaji wao kutoka nchini Uganda Emmanuel Arnold Okwi aliyeanza kulisabahi lango la Mbeya City katika dakika ya 20.

Bao la pili la Simba lilikwamishwa kimiani na beki kutoka nchini Ghana Asante Kwasi dakika ya 36, kwa kuunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Shiza Ramadhani Kichuya.

Hata hivyo Mbeya City walifanikiwa kupata bao la kufutia machozi katika dakika ya 37, kupitia kwa mshambuliaji wao Frank Ikobela aliyeunganisha kwa kichwa kona ya Danny Joram.

Dakika moja baadae Simba waliongeza bao la ushindi lililofungwa na nahodha mshambuliaji John Raphael Bocco akimalizia krosi ya beki Shomary Kapombe kutoka upande wa kulia.

Ushindi huo unawafanya Wekundu hao wa Msimbazi wafikishe alama 55 baada ya kushuka dimbani mara 23, huku wakiendelea kuwatimulia vumbi mahasimu wao katika soka la bongo Young Africans wenye alama 47 na michezo 22.

Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Aprili 13, 2018
Mtibwa Sugar yawika mashamba ya miwa

Comments

comments